Wafanyakazi wakisimama kwenye lango la mgodi wa Gold One. / Picha: Reuters

Baadhi ya wachimba migodi ambao walikaa ndnai ya machimbo ardhini kwa zaidi ya siku mbili katika mzozo kati ya vyama pinzani vya wafanyakazi wa Afrika Kusini walianza kurejea juu siku ya Jumatano, wawakilishi wao walisema.

Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi wa Migodi (NUM), moja ya vyama viwili vilivyohusika, kilisema wafanyakazi 107 kati ya zaidi ya 500 ambao walishindwa kutoka kwenye mgodi wa Gold One huko Springs, Mashariki mwa Johannesburg, baada ya zamu ya Jumatatu asubuhi " wameanza kutokea nje ya machimbo".

"Kwa sasa wako katika kituo cha matibabu kwa uchunguzi zaidi," msemaji wa NUM Livhuwani Mammburu aliambia AFP.

NUM na wasimamizi katika mgodi huo walidai wafanyakazi walikuwa "wanashikiliwa mateka" na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Ujenzi (AMCU), ambacho ni chama pinzani.

'Watekaji walizidiwa nguvu'

AMCU ilikanusha madai hayo ikisema wachimba migodi walikuwa wakifanya maandamano ya "kukaa ndani".

"Nimeambiwa waliwazidi nguvu wale waliokuwa wakiwashikilia mateka na wakakimbia," Mammburu, afisa wa chama cha NUM alisema kuhusu 107 waliojitokeza Jumatano.

Vikosi vya uokoaji na usalama vilikuwa vinafanya kazi ili kuwatoa wachimba migodi waliosalia, alisema.

Katibu wa kanda wa AMCU Tladi Mokwena alikanusha maelezo haya, akisema wachimbaji madini wote walikuwa wakitoka "kwa hiari" wakiwa wamekosa chakula.

"Uongozi umefunga njia zote za kupokea chakula. Kwa hiyo, hatukuweza kuruhusu wafanyakazi kukaa chini ya ardhi bila chakula," alisema.

Polisi hawakujibu mara moja ombi la maoni.

Siku ya Jumanne, msemaji wa polisi Dimakatso Nevhuhulwi alisema maafisa walikuwa "wamewekwa tayari '' na wanafuatilia hali hiyo huku mazungumzo kati ya mgodi huo na vyama vya wafanyakazi yakiendelea.

Doria ya usalama

Mwandishi wa AFP Jumanne jioni alisema polisi na vikosi vya usalama vilishika doria katika eneo hilo huku wachimba migodi wapatao 100, wengi wao kutoka AMCU, wakiimba nyimbo za maandamano huku wakisubiri matokeo ya mkutano kati ya usimamizi wa mgodi na vyama vya wafanyakazi.

Mzozo unahusu uwakilishi wa vyama vya wafanyakazi kwenye mgodi, ambapo kwa sasa NUM ndio kundi pekee lililosajiliwa rasmi.

AMCU inasema idadi kubwa ya wachimba migodi wamejiandikisha kujiunga nayo. Lakini bado haijapewa uwakilishi rasmi, ambayo inasema ndio sababu ya maandamano hayo.

NUM ilianzishwa mwaka 1982 na Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa, mwanaharakati wa zamani wa chama cha wafanyakazi. Inasalia kuwa chama kikuu cha wafanyakazi wa migodini nchini.

TRT Afrika