Joan E Donoghue, rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, alisoma uamuzi uliosubiriwa kwa hamu na jopo la majaji 17. Picha: Reuters 

Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa imeiamuru Israeli kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki katika agizo lake la muda siku ya Ijumaa pia iliiamuru Israel kuboresha hali ya kibinadamu katika eneo lililozingirwa.

Mahakama ilisema ina mamlaka ya kutoa uamuzi juu ya hatua za dharura, na kuongeza kwamba haitatupilia mbali kesi ya mauaji ya halaiki kama Israeli ilivyoomba.

Imebainisha kuwa Wapalestina wanaonekana kuwa kundi linalolindwa chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, na kusisitiza kuwa inatambua haki ya Wapalestina huko Gaza kulindwa dhidi ya vitendo vya mauaji ya kimbari.

Serikali ya Afrika Kusini, ambayo iliwasilisha kesi katika mahakama hiyo, ilisema "inatumai kwa dhati kuwa Israeli haitafanya kazi ya kutatiza utekelezwaji wa amri hiyo."

Ushindi wa uhakika

"Leo ni ushindi mnono kwa utawala wa sheria wa kimataifa na hatua muhimu katika kutafuta haki kwa watu wa Palestina," Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ilisema.

Tarehe 29 Disemba, Afrika Kusini ilienda kotini kuomba amri ya Israeli kuzuiwa ikidai kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanakiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.

Miongoni mwa hatua ambazo Afrika Kusini iliomba ni kusitishwa mara moja kwa mashambulizi ya kikatili ya Israel, ambayo yameharibu sehemu kubwa ya eneo hilo na kuua zaidi ya Wapalestina 26,000, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza.

Pia iliomba ICJ itoe amri ya kuizuia Israel kutokana na uharaka wa hali hiyo.

Baada ya mashtaka kuwashilishwa Januari 11-12, mahakama ilianza mashauri baada ya kuchunguza hoja na ushahidi wa pande zote.

TRT Afrika