Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ni miongoni mwa wakuu wa nchi za Afrika wanaoshiriki katika mkutano wa Paris. Picha: Reuters

Takriban viongozi 14 wa Afrika ambao wako Paris, Ufaransa kwa mkutano wa siku mbili wanashinikiza kuwepo kwa mpango mzuri wa ufadhili ili kuimarisha maendeleo katika bara hilo.

Njia zinazowezekana za kukabiliana na umaskini, ongezeko la joto duniani na uhifadhi wa mazingira ni maeneo ya kipaumbele katika mkutano wa Juni 22-23.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema masuala yote mawili - mabadiliko ya tabia nchi na kutokomeza umaskini - ni muhimu, na kwamba nchi "hazipaswi kuchagua kati ya kupunguza umaskini na kuhifadhi mazingira."

Miongoni mwa marais wa Afrika wanaoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Bola Tinubu wa Nigeria, Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), William Ruto (Kenya) na Kais Saied (Tunisia).

Marais kutoka Benin, Senegal, Gabon, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Comoro, Mauritania na Togo pia wanahudhuria.

Usanifu wa fedha

Mkutano huo pia unatarajia kuweka msingi wa marekebisho ya usanifu wa fedha wa kimataifa ulioanzishwa na nchi za Magharibi baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Waziri Mkuu wa China Li Qiang anatarajiwa kuzungumza juu ya suluhu za kurekebisha madeni ya nchi maskini zaidi duniani.

Ahadi 'tupu'

Mwanaharakati wa mabadiliko ya tabia nchi wa Uganda Vanessa Nakate alihutubia wajumbe baada ya Rais Macron kuzindua semina hiyo siku ya Alhamisi.

Aliwataka wasikilizaji kuzingatia dakika moja ya ukimya kwa watu walioathiriwa na maafa. Nakate alikashifu sekta ya mafuta kwa "kutoa ahadi tupu kwa nchi zinazoendelea."

Pia alishutumu nchi "tajiri zaidi" kwa kuongeza utajiri wao kwa kuhujumu mageuzi muhimu ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi.

"Tafadhali, usituambie kwamba tunapaswa kukubali hewa yenye sumu na mashamba yaliyokauka na maji yenye sumu ili tupate maendeleo," Nakate alisema.

Washiriki pia watapitia upya ahadi iliyotolewa na mataifa yenye nguvu mwaka 2009 kwamba dola bilioni 100 zitatolewa kila mwaka kufadhili hatua za kuhifadhi hali ya hewa katika mataifa yanayoendelea.

TRT Afrika