Ujumbe wa viongozi wa Afrika unatarajiwa mjini St Petersburg Jumamosi kwa mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin kama sehemu ya "ujumbe wao wa amani" wa kumaliza vita nchini Ukraine.
Wajumbe hawa ni marais wa Afrika Kusini, Senegal, Comoros, na Zambia. Marais wa Misri, Jamhuri ya Kongo na Uganda walituma wawakilishi.
Walikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, mjini Kyiv siku ya Ijumaa.
"Kwa maoni yetu ni muhimu kusikiliza kwa makini kile ambacho nchi zote mbili zinasema, " rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alisema Ijumaa.
Alisisitiza "kuwe na amani kupitia mazungumzo".
Lakini rais Zelensky alikataa uwezekano huo wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na wajumbe hawa.
"Nilisema wazi mara kadhaa katika mkutano wetu kwamba kufanya mashauriano yoyote sasa na Urusi, ilhali wametuvamia na kunyakua ardhi yetu, ni kuendeleza vita, kuendeleza unyanyasaji na mateso." Amesema Zelensky
Katika taarifa yake, Zelensky aliwashauri viongozi hao kuangazia maoni yao kwa njia za kukomesha "uhalifu unaofanywa na Urusi", na jinsi ya kushughulikia usalama wa chakula.
Bei za nafaka
Bara la Afrika limeathiriwa vibaya na kupanda kwa bei ya nafaka na mbolea pamoja na athari kubwa kwa biashara ya kimataifa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka jana.
"Mgogoro huu pia unaathiri vibaya nchi za Afrika, ukigusa maisha ya watu bilioni 1.2 au 1.3 katika bara hili," Ramaphosa alisema.
Mataifa ya Afrika yamegawanyika kuhusu vita hivyo, huku baadhi wakiegemea upande wa Ukraine na wengine wakichagua imma kutoegemea upande wowote, au kuegemea Moscow.