Fidan ameashiria umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja za nishati na kijeshi. / Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alitangaza kwamba alijadiliana na mwenzake wa Macedonia Kaskazini, Timco Mucunski, kuhusu uwezekano wa kuanzishwa kwa 'Baraza la Ushirikiano wa Kimkakati wa Ngazi ya Juu' ili kurasimisha na kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Fidan alisisitiza kuwa Uturuki imewasilisha nia yake kuhusu suala hilo, akibainisha kuwa Uturuki inalenga kuinua ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili ili kuendana na kiwango cha uhusiano wao wa kisiasa.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uturuki alisisitiza kuwa lengo ni kuongeza kiwango cha biashara kati ya Uturuki na Macedonia Kaskazini hadi dola bilioni 2 na akataja kuwa yeye na Mucunski wamejadili hatua za kufikia lengo hilo.

Alisema kuwa Uturuki inafuatilia kwa karibu matukio ya Macedonia Kaskazini na kuongeza kuwa anaamini maendeleo yataongezeka katika kipindi kipya cha serikali.

Ushirikiano wa nishati na kijeshi

Akibainisha umuhimu wa ushirikiano wa nishati na kijeshi kati ya nchi hizo mbili, Fidan alisema: “Ninaamini kuwa masuala kama vile mafunzo ya kijeshi na kushiriki katika mazoezi ya kijeshi yatapata kasi kubwa katika kipindi kijacho. Makampuni ya sekta ya ulinzi katika nchi yetu vinaongoza duniani na ningependa kusisitiza kwamba makampuni haya yako tayari kutoa mchango wake kwa Macedonia Kaskazini."

Akisema kuwa Macedonia Kaskazini ina nafasi ‘maalum’ kwake, Fidan alitaja umuhimu wa vitu vya sanaa vya Ottoman nchini humo na kwa utajiri wa kitamaduni wa Macedonia Kaskazini.

Kusaidia mipango ya kitamaduni

Fidan alibainisha kuwa kazi za ukarabati zilizofanywa kupitia msaada wa taasisi za Kituruki zimekuwa vivutio kuu vya watalii na alionyesha kuridhika na maendeleo haya.

Pia alisisitiza kuwa msaada kwa mipango ya kitamaduni utaendelea bila kupungua katika kipindi kijacho.

Akitoa shukrani kwa ukarimu wa mwenzake wa Macedonia Kaskazini, Fidan alibainisha kuwa ametembelea Macedonia Kaskazini na Skopje mara nyingi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita katika nyadhifa mbalimbali.

Fidan pia aliipongeza Macedonia Kaskazini kwa serikali yake mpya, akisema: "Uturuki imekuwa ikiunga mkono Masedonia Kaskazini tangu ipate uhuru na itaendelea kufanya hivyo."

TRT World