Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Mafuta ya mawese yanapatikana katika takriban kila kitu tunachotumia, hii ni kunzia mafuta ya kupikia, bidhaa tunazonunua kama pizza, donati na chokoleti, hadi kiondoa harufu yaani deodorant, shampoo, dawa ya meno na lipstick.
Inatumika pia katika malisho ya wanyama na kama nishati ya mimea katika sehemu nyingi za ulimwengu.
Mafuta ya mawese pia yanaweza kutumika kama mafuta katika injini za dizeli.
Afrika ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa mafuta haya baada ya Kusini-mashariki mwa Asia.
Nigeria inaongoza kwa uzalishaji wa zaidi ya tani metriki milioni 1.4, ikiifanya nchi ya tano kwa ukubwa duniani kwa uzalishaji wa mafuta ya mawese na mzalishaji mkuu barani Afrika.
Inafuatiwa na Côte d'Ivoire na zaidi ya tani 600,000, Cameroon zaidi ya tani 460,000 na Ghana na DRC zikizalisha zaidi ya tani 300,000.

Katika eneo letu la Afrika Mashariki, Tanzania inazalisha mafuta ya mawese katika maeneo ya Kigoma, Mbeya and Pwani.
Huko Uganda, kilimo cha mawese kinafanyika katika eneo la Kalangala ambapo kampuni kubwa ya mafuta ya kigeni imewekeza.
Michikichi barani Afrika inakadiriwa kulimwa kwa zaidi ya ekari milioni 14, kilimo kikiongozwa na wakulima wadogo wadogo.Mnamo mwaka wa 2020, uzalishaji wa mafuta ya mawese Afrika ulifikia zaidi ya tani milioni 13, hii ikionyesha ukuaji chanya ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Michikichi ya mafuta huchukua takribani miezi 30 kufikia ukomavu, wakati huo wafanyakazi kwenye mashamba hayo huanza kuvuna.Utaratibu unaweza kurudiwa kila siku saba hadi kumi.
Kwa kutumia mundu mrefu, vishada vya matunda mapya ya mitende ya mafuta huondolewa.Mikungu iliyo tayari kuvunwa inaweza kutambuliwa kwa rangi yao ya machungwa.

Mara tu matunda yanapovunwa, ni wakati wa mchakato wa utengenezaji.Sehemu mbili tofauti za mazao hutumiwa kwa bidhaa zilizotengenezwa kutoka kwa mazao - matunda na punje.
Nchi za Ulaya na Asia ndizo wanunuzi wakuu wa mafuta ya mawese barani Afrika, huku nchi kama Uholanzi, Ubelgiji, India, na Uchina zikiongoza kwa uagizaji kutoka nje.
Lakini licha ya uzalishaji mkubwa barani bado Afrika inanunua mafuta ya mawese kutoka nje.
Mataifa ya Afrika yaliagiza karibu tani milioni 8 za mafuta ya mawese mwaka 2020, kulingana na taarifa kutoka Shirika la Kilimo na Chakula FAO.

Kwa mfano, Nigeria ambayo ndio mzalishaji mkubwa wa mafuta ya mawese, lakini bado inaongoza kuagiza kutoka nje. Mwaka 2020 iliagiza zaidi ya tani milioni 1.2 za mafuta ya mawese.
Changamoto kubwa iko katika ukosaji wa uboreshaji wa mafuta ya mawese barani na hivyo wakulima wadogo wadogo kutonufaika.
Makampuni ya kigeni yanalima michikichi barani kwa ajili ya biashara zao na hapo inaleta changamoto ya wakulima kukata miti wakitaka kunufaika kwa miradi hii.
Wataalamu wanasema kujenga viwanda barani vya kuboresha mafuta ya mawese, kumpa usaidizi mkulima mdogo wa michikichi na kuweka sera za kuwatetea katika kilimo hiki kutasaidia kuinua faida ya wale wanaoinua fahari hii ya Afrika .