Urusi imesema kuwa inaelewa wasiwasi ambao mataifa ya Afrika yanaweza kuwa nayo baada ya Moscow kuachana na mkataba wa nafaka wa Ukraine, na imeahidi kuhakikisha nchi zenye mahitaji yanafikishiwa nafaka zinazohitaji.
Nchi kumi barani Afrika zimekuwa zikipokea nafaka kutoka Ukraine chini ya mkataba wa Bahari Nyeusi . Mkataba huu umeiwezesha Ukraine kuendelea kuuza nafaka licha ya vita kuendelea.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Vershinin aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba nchi zinazohitaji msaada zitapata hakikisho muhimu katika mkutano wa marais baadaye mwezi huu,
"Tunaelewa wasiwasi ambao marafiki zetu wa Afrika wanaweza kuwa nao," Vershinin alisema. "Lakini nataka kusema kwamba wasiwasi huu sio tu unaeleweka lakini utazingatiwa kikamilifu."
"Nchi zinazohitaji wakati wa mawasiliano nasi na wakati wa mkutano ujao wa marais wa Russia-Afrika kwa kawaida zitapokea hakikisho kuhusu mahitaji yao ya mazao ya kilimo - kwanza kabisa nafaka," aliongeza.
Mkutano wa marais kati ya Urusi na Afrika unatarajiwa kufanyika katika mji wa pili wa Urusi wa Saint Petersburg mwishoni mwa Julai, shirika la habari la AFP linaripoti.
Urusi kujiondoa kwa makubaliano ya nafaka
Maoni ya Vershinin yalikuja siku chache baada ya Urusi kujiondoa katika makubaliano ya kihistoria ya nafaka ambayo yaliruhusu kwa meli za mizigo zilizobeba nafaka za Ukraine kutoka bandari za Bahari Nyeusi, kupita kwa usalama.
Moscow kwa muda wa miezi kadhaa ililalamika kwamba makubaliano yanayohusiana na kuruhusu usafirishaji wa chakula na mbolea ya Kirusi hayakuheshimiwa.
Rais wa Urusi Vladimir Putin wiki hii alisema kuwa Urusi itafikiria kurejea katika makubaliano hayo iwapo matakwa yake yatatimizwa "kikamilifu" akisema makubaliano hayo "yamepoteza maana ".
Vershinin aliwaambia waandishi wa habari kwamba kwa sasa "hakuna mawasiliano" kutafuta njia mbadala ya mpango wa nafaka.
Mkataba huo wa nafaka, uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, ulikuwa umewezesha mauzo ya nje ya zaidi ya tani milioni 32 za nafaka za kutoka Ukraine katika mwaka uliopita.