Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, linasema "Wengi wa watu wana njaa" nchini Sudan wakati nchi hiyo ikielekea kuporomoka baada ya miezi kumi ya vita.
"Kwa wakati huu, chini ya asilimia tano ya Wasudan wanaweza kumudu mlo wa kwa siku," mkurugenzi wa nchi wa Sudan wa WFP, Eddie Rowe, aliwaambia waandishi wa habari mjini Brussels.
Tangu Aprili mwaka jana, Sudan imekuwa ikishikiliwa na mapigano kati ya jeshi la kawaida na Vikosi vya Rapid Support Forces, ambayo yameua maelfu ya watu na kuunda kile Umoja wa Mataifa unakiita "mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani."
Kwa pamoja watu milioni 10.7 wamelazimishwa kuhama makwao kwa sababu ya vita na migogoro kulingana na Umoja wa Mataifa.
Maafa ya kibinadamu
Watu milioni tisa wamesalia kuwa wakimbizi ndani ya Sudan, ambapo Rowe alisema kwa sababu ya "migogoro mibaya inayoendelea, mavuno yaliyokwama, na hatari kubwa ya kuhama makazi yao kuwatumbukiza mamilioni zaidi katika janga kubwa la kibinadamu."
Kote Sudan, ambayo WFP inasema tayari ilikuwa inakabiliwa na moja ya mgogoro mbaya zaidi wa chakula duniani kabla ya vita, watu milioni 18 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Kati ya hao, Rowe alisema "karibu milioni tano wako kwenye kilele cha janga." Mashirika ya misaada yameonya kwa miezi kadhaa kwamba, kutokana na kukwamishwa kwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na ufadhili mdogo wa fedha, hali ya njaa inaikabili Sudan.
Lakini vikwazo vile vile vya utoaji wa misaada hasa kwa maeneo yenye vita, huzuia uwezo wa kutoa msaada kwa wanaohitaji.