RSF imeshutumiwa kuwabaka na kuwalazimish abaadhi ya wanawake kubeba mimba kwa ajili ya kuzaa watoto wa Kiarabu/ Picha: Reuters 

Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) na washirika wake wamefanya viwango vya "kushangaza" vya unyanyasaji wa kingono, kuwabaka raia huku wanajeshi wakisonga mbele na kuwateka nyara baadhi ya wanawake kama watumwa wa ngono wakati wa vita vilivyodumu zaidi ya miezi 18, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne.

Waathiriwa wameanzia kati ya miaka minane hadi 75, ilisema ripoti ya ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, huku unyanyasaji mwingi wa kingono ukifanywa na RSF na wanamgambo washirika wa Kiarabu katika jaribio la kuwatisha na kuwaadhibu watu kwa kushukiwa kuwa na uhusiano na maadui.

"Kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kijinsia ambao tumerekodi nchini Sudan ni cha kushangaza," mwenyekiti wa misheni Mohamed Chande Othman alisema katika taarifa iliyoambatana na ripoti ya kurasa 80 iliyofuatia mahojiano na waathiriwa, familia na mashahidi.

Ripoti hiyo ilirejea uchunguzi wa Reuters na makundi ya haki za binadamu kuhusu unyanyasaji mkubwa wa kingono katika mzozo huo.

RSF, ambayo inapambana na jeshi la Sudan, haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.

Hapo awali ilisema itachunguza tuhuma na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Uhasama wa kulenga makabila

Wanajeshi wa RSF wana mizizi katika kile kinachoitwa wanamgambo wa Janjaweed, ambao walisaidia wanajeshi kukomesha uasi katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan miongo miwili iliyopita.

Katika mzozo wa sasa, RSF imechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya Sudan ikiwa ni pamoja na Darfur Magharibi ambako inashutumiwa kutekeleza mauaji ya kikabila dhidi ya watu wa Masalit kwa msaada wa wanamgambo wa Kiarabu.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulisema maneno ya kibaguzi dhidi ya watu wasio Waarabu katika sehemu za jimbo la Darfur Magharibi yalitumiwa sana wakati wa mashambulizi ya kingono, kuashiria kulenga makabila.

Walazimishwa kubeba mimba

Mwathiriwa mmoja kutoka El Geneina huko Darfur Magharibi alisema mbakaji wake alimwambia akiwa amemnyooshea bunduki: "Tutakufanya, wasichana wa Masalit, kuzaa watoto wa Kiarabu," ripoti hiyo ilisema.

Katika kesi nyingine, mwanamke wa Darfur Magharibi alishikiliwa mateka kwa zaidi ya miezi minane na walinzi wa RSF na kupewa mimba na mshikaji wake mkuu wakati wa ubakaji wa mara kwa mara, iliongeza.

Katika matukio mengine manne, wanawake walichukuliwa kutoka mitaani kabla ya kupigwa na kubakwa kisha kuachiliwa au kutelekezwa mitaani wakiwa wamepoteza fahamu.

Wahalifu mara nyingi walivaa sare za RSF au mitandio iliyoficha nyuso zao, waathiriwa walisema.

Reuters