Mzozo wa Sudan umesababisha uharibifu katika maeneo mengi hasa mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum/ Photo: AA

Na Coletta Wanjohi

Kabla ya Mkutano wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 15 na 16 Februari, Tume ya Umoja wa Afrika imetathmini hali nchini Sudan.

Mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF nchini humo yanaendelea tangu Aprili 2023.

"Sudan ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa Umoja wa Afrika na kama shirika, tunaweka juhudi zetu zote mbele kutatua mgogoro wa Sudan," Amb. Bankole Adeoye Kamishna wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama anasema.

Adeoye alikuwa akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu, mjini Addis Ababa, Ethiopia, uliojitolea kujadili mgogoro wa Sudan.

Uliandaliwa na taasisi ya kuzingatia haki na demokrasia ya Umoja wa Afrika AGA, utaratibu wa AU uliopewa jukumu la kukuza utawala bora.

Sudan haitahudhuria mkutano wa AU ingawa suala la nchi hiyo litakuwa moja ya mada zitakazojadiliwa na wakuu wa nchi za Afrika.

Uanachama wake umesitishwa kwa muda na Umoja wa Afrika kwa kutokuwa na uongozi wa kiraia.

"Ufanisi wa vikwazo na Umoja wa Afrika mara nyingi unatiliwa shaka kutokana na migogoro inayoendelea na ukiukwaji wa haki za binadamu katika bara zima. Suala la msingi ni utekelezaji dhaifu," Nuur Mohamud Sheekh, mchambuzi na msemaji wa zamani wa shirika la IGAD, aliiambia TRT Afrika.

Dkt. Mohamed Ibn Chambas mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya Juu la Umoja wa Afrika kuhusu Sudan/ picha : AU 

Sheekh anasema AU lazima ianzishe chombo maalum cha utekelezaji chenye mamlaka ya kufuatilia uzingatiaji na kutoa adhabu kwa nchi ambazo zinakwenda kinyume na matarajio yake.

"Vikwazo vinatakiwa kuwa hatua ya mwisho kabisa. Mazungumzo na diplomasia ndizo njia zinazopendekezwa kutatua migogoro kwa amani kwa sababu athari za vikwazo huumiza zaidi raia wa nchi zinazolengwa,” Sheekh anaiambia TRT Afrika.

Juhudi za amani za Umoja wa Afrika zinaendelea kuhimiza wadau wa Sudan kuacha mapigano.

"Tabaka la kisiasa limegawanyika pakubwa hata hivyo, lazima tusitishe vita nchini Sudan kwa sababu vinatuathiri sisi sote. Hivi sasa, Sudan Kusini, Ethiopia, Misri, Chad zinahifadhi maelfu ya wakimbizi. Vita nchini Sudan pia ni vita katika Pembe ya Afrika,” Kamishna Bankole anaongeza.

Hali kwa raia nchini humo inazidi kuzorota huku mapigano yakiendelea.

"Idadi ya wakimbizi wa ndani iliongezeka mwaka 2024, kutoka milioni 9 hadi milioni 11.5, huku watoto wakiwa zaidi ya 53% ya waliokimbia makazi yao," anasema Wilson Almedia Adao, mwenyekiti wa Kamati ya Afrika ya wataalam wa Haki na Ustawi wa Mtoto.

Juhudi za upatanishi

"Huu ni hali mbaya zaidi kwa watu duniani," anasema Dkt. Mohamed Ibn Chambas mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya Juu la Umoja wa Afrika kuhusu Sudan.

Dkt. Chambas anaongoza Jopo la Ngazi ya Juu la Umoja wa Afrika kuhusu Sudan (HLP-Sudan).

Pia inawajumuisha Dkt. Specioza Wandira-Kazibwe, Makamu wa Rais wa zamani wa Uganda na Balozi Fransisco Madeira, Aliyekuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti Somalia na Aliyekuwa Mkuu wa ATMIS.

Jopo hilo lilianzishwa na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat, na lilianza kazi yake tarehe 31 Januari 2024 kufanya kazi pamoja na taasisi za Sudan ili kupata suluhu ya kumaliza mapigano.

"Juhudi za kutatua mgogoro bado hazijafanikiwa lakini kama Umoja wa Afrika, bado tuna ya kumaliza mgogoro," anasema Dkt. Chambas.

AU inasema ni mazungumzo ya kisiasa kati ya watu wa Sudan wenyewe, wala sio makabiliano ya kijeshi yatakayoweza kumaliza vita hivi.

"Juhudi za upatanisho za AU zinaongozwa na dira ya AU kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Sudan ambao unahitaji Sudan kuongoza juhudi za amani, " anasema Dkt. Chambas.

Miguel Ntuntumu Evuna Andeme, Balozi wa Equatorial Guinea na Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Februari 2025 anasema kuzuia migogoro na kukuza utawala bora "kunahitaji mabadiliko ya mawazo na kujitathmini kwa kina kuhusu wapi tumekosea."

Viongozi wa Afrika watakapokutana tarehe 15 na 16 Februari, wataamua hatua zinazofuata za kurejesha utulivu nchini Sudan.

TRT Afrika