Umoja wa Afrika wafanya mkutano kutafakari mapinduzi ya serikali

Umoja wa Afrika wafanya mkutano kutafakari mapinduzi ya serikali

Niger , Burkina Faso, Guinea, Mali, Sudan na Gabon ziko chini ya uongozi wa kijeshi.
Umoja wa Afrika umefanya mkutano wake wa pili wa kujadili kuhusu bara na mapinduzi ya serikali Afrika. / Picha: Umoja wa Afrika 

Umoja wa Afrika umefanya mkutano wake wa pili wa kujadili kuhusu bara na mapinduzi ya serikali Afrika.

Mkutano huo uliofanyika mjini Accra nchini Ghana kutoka 18 had 19 Machi 2024, umeandaliwa na Tume ya AU ya Amani na Usalama. Hii ni mara ya pili ya mkutano aina hii kufanyika, wa kwanza ulikuwa mwaka 2023.

"Tulipokusanyika hapa miaka miwili iliyopita, nchi nne wanachama wa muungano wetu zilikuwa zimesimamishwa kutokana na kutokea kwa mapinduzi ya kikatiba ya serikali katika maeneo yao. Hali ilikuwa mbaya sana, hivyo mkutano wetu, hapa Accra, ulikuwa wa lazima," Rais wa Ghana Akuffo Adoo alisema akifungua mkutano huo.

"Leo, miaka miwili baadaye, hali imekuwa mbaya zaidi. Tunapokusanyika hapa, nchi sita wanachama wa Muungano wa Umoja wa Afrika zimesimamishwa kwa sababu hizo hizo," Raid Akuffo Ado aliongezea.

Niger , Burkina Faso, Guinea, Mali, Sudan na Gabon ziko chini ya uongozi wa kijeshi.

Kati ya mapinduzi 9 yaliyoshuhudiwa barani Afrika kati ya 2020 na 2023, sita yalifanyika Afrika Magharibi pekee. Mbali na mapinduzi haya, kumekuwa na majaribio mengine ya mapinduzi ndani ya wakati huo huo katika mataifa kadhaa wanachama wa AU.

"Kuibuka upya kwa mapinduzi ya serikali kunachukuliwa kwa kiasi kikubwa kunatokana na wasiwasi kuhusu ukosefu wa ushirikishwaji na uwajibikaji katika michakato ya utawala na kufanya maamuzi," Damtien Tchintchibidja, makamu wa rais wa Tume ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, aliambia mkutano huo.

"Wananchi katika nchi wanachama zilizoathiriwa waliwakaribisha viongozi wa kijeshi kwa shangwe, wakiamini kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuleta hali bora zaidi," aliongezea.

Katiba ya Umoja wa Afrika inasema kuwa nchi ambayo inafanya mapinduzi ya serikali itasimamishwa uanachama wa Umoja wa Afrika hadi hapo itakapofanya uchaguzi na rais kuchukua uongozi.

"Iwapo tutashindwa kuzingatia matakwa na matarajio halali ya wananchi wetu, au kuendelea kuchezea katiba zetu, tutaendelea kutengeneza nafasi kwa ajili ya maasi ya wananchi wengi zaidi, kuchukua madaraka ya kijeshi na aina nyingine za mabadiliko ya serikali kinyume na katiba ya bara letu," Emilia Mkusa balozi wa Namibia katika AU alisema.

"Haya yote yatatokana na kukatishwa tamaa kwa wananchi, ambao wanashindwa kutafuta njia muafaka za kushughulikia matatizo yao," aliongezea.

Mkutano wa kwanza kujadili hali ya mapinduzi barani ulifanyika Ghana Machi 2022 na hadi sasa AU haijapata suluhisho la kudumu la kusimamisha mabadaliko hayo yasiyo halali.

TRT Afrika