Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat anasema kuanguka kwa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi kutaathiri mamilioni ya Waafrika. Picha: Reuters

Tume ya Umoja wa Afrika imesema "inasikitika" kutokana na kushindwa kutiliwa saini kwa Mkataba wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao umenufaisha mamilioni ya watu duniani kote tangu kuanzishwa kwake mwaka mmoja uliopita.

"Najuta kusitishwa na kusimamishwa kwa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi ambao Umoja wa Afrika umekuwa mstari wa mbele wa kuutetea ili utekelezaji wake uanze mara moja. Ninaziomba pande husika kusuluhisha masuala yoyote ili kuanza tena upitishaji salama wa nafaka na mbolea kutoka Ukraine na Urusi hadi sehemu bidhaa hizo zinapohitajika, hasa katika bara la Afrika,”

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alisema katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumanne.

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao unaruhusu kupita kwa usalama kwa meli zinazobeba nafaka na mafuta kutoka Ukraine iliyokumbwa na vita, ulikwama siku ya Jumatatu baada ya Urusi kukataa kutia saini utekelezaji wake.

Mkataba huo ambao ulihitaji saini kutoka kwa mataifa ya - Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa (UN) ambao ili uweze kuanza utekelezaji wake lazima pande zote zitie saini ili mkataba wa nafaka uweze kuongezwa muda kwenye utekelezaji wake. Nchi ya Urusi imeeleza kuwa moja ya sababu kubwa ni "kutokuwa na haki" katika pande zote.

Urusi inataja "kutokuwa na haki"

Ukweli ni kwamba Pande zote isipokuwa Urusi zilikuwa zimeelezea kujitolea kwao kuendeleza mpango huo.

Kremlin inashutumu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ambayo yangeruhusu Urusi kuuza nje mbolea na chakula chake licha ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi.

Uturuki ambayo ina njia muhimu ya kupita kwa meli zinazoingia na kutoka katika eneo la nchi ya Ukraine ilikuwa imeelezea matumaini kuwa Urusi itakubali kuanzishwa upya kwa mkataba huo wa nafaka.

Angalau nchi kumi za Kiafrika, hasa zile za Pembe ya Afrika, zilikuwa zikinufaika kwa Asilimia kubwa na Mkataba wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Shashwat Saraf, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji, awali aliiambia TRT Afrika kwamba kushindwa kurejea kwa mkataba wa nafaka kumesababisha "kuyumba kwa soko la chakula duniani."

“Nchi nyingi za Afŕika Mashaŕiki na sehemu nyingine za dunia zinategemea uagizaji wa chakula ili kupunguza uhaba katika soko la ndani. Ikiwa suluhu ya mpango wa nafaka haitapatikana, uhaba wa chakula katika mataifa yanayoendelea utazidi kuwa mbaya zaidi," Saraf alisema.

Abdikadir Bille, mkulima na mhusika mkuu katika sekta ya kilimo nchini Somalia, pia alikuwa ametabiri nyakati ngumu zaidi kwa Afrika kama mpango huo utasambaratika.

“Kutokana na ukame wa muda mrefu katika eneo la Pembe ya Afŕika, mamilioni ya watu wamekabiliwa na mgogoŕo wa njaa. Nina matumaini pande husika zitaongeza muda wa mpango wa Mkataba wa nafaka ili kuepusha hali utapiamlo na vifo vinavyosababishwa na njaa,” alisema kabla ya kukamilika kwa mpango huo wa nafaka mnamo Julai 17.

‘Kuepusha utapiamlo na vifo’

Wanufaika wakuu wa Mkataba wa Nafaka wa Bahari Nyeusi barani Afrika ni Misri, Tunisia, Kenya, Ethiopia, Algeria, Sudan, Libya na Somalia, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Nchi nyingi hupokea ngano, mahindi, maharagwe ya soya, mafuta ya alizeti na shayiri kutoka Ukraine.

Reuters