Mamlaka ya Uganda inachunguza tuhuma za sumu kwa chakula baada ya wanafunzi 150 kupelekwa hospitalini.
Wanafunzi hao wanasemekana walianza kulalamikia maumivu ya tumbo baada ya mlo wao wa jioni siku ya Jumatano katika Shule ya Sekondari ya Nakanyonyi wilayani Mukono katikati mwa Uganda.
Wanafunzi hao 150 walikuwa katika hospitali ya Wilaya, hakuna vifo vilivyorekodiwa. Wengi wao wamepokea matibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani, msemaji wa polisi Patrick Onyango aliiambia TRT Afrika.
"Hivi tunavyozungumza sasa, ni 10 pekee ambao bado wamelazwa," alisema.
'Wanafunzi walilazwa hospitalini, inashukiwa kulikuwa na sumu kwenye chakula. Waliruhusiwa jana kuondoka hospitalini (Alhamisi) lakini wengine walipata matatizo tena usiku na wakakimbizwa hospitalini,'' aliongeza.
Mamlaka inasema wamechukua sampuli za chakula kwa uchunguzi wa kimatibabu lakini wengi wa wanafunzi walikuwa bado katika hali ''hatari'' baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Alisema polisi bado wanafuatilia hali hiyo ''wakiwa na magari mawili yenye wagonjwa yakiwa yamesimama shuleni.''
'"Tumechukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi ili kuthibitisha kama chakula chake kilikuwa na sumu ,'' Onyango alisema.