Wakati habari zilipoibuka za mapigano nchini Sudan macho yote yalielekea huko.
Waliokuwa ndani ya Sudan au nje kila mtu alifuata matukio ya machafuko jinsi yalivyotokea.
Ni kutokana na juhudi za waandishi wa habari waliojitokeza na kuweka maisha yao katika mstari wa mbele kuujulisha ulimwengu kile kilichokuwa kikiendelea.
‘’Nilipewa saa mbili na mhariri wangu kufika uwanja wa ndege na kwenda Sudan kwa ajili ya kuripoti matukio. Ilikuwa ni habari motomoto wakati huo.’’ Anasema Hassan Majid, mwandishi wa habari wa video anayeishi Nairobi. ‘’Mwisho wa siku hiyo nilikuwa Khartoum tayari kuwasilisha.’’
Na ndivyo ilivyo kwa hadithi nyingine yoyote kubwa.
Jukumu la Vyombo vya Habari
Lakini Vita inategemea sana ripoti zinazotolewa. Jinsi matukio yanavyoripotiwa hutoa mtazamo juu ya jinsi mambo yalivyo mabaya, au ni nani anayeshindwa na nani anashinda katika vita.
‘’Jukumu la vyombo vya habari ni kuripoti jinsi ilivyo na pia kuvuta hisia za umma na kuwajuza ikiwa ni pamoja na jumuiya ya kimataifa, kinachoendelea.’’ Anasema Mtaalamu wa Usalama Dkt, Adams Bornah.
‘’Katika hali ya vita vyombo vya habari vinapaswa kuwa na jukumu lisiloegemea upande wowote na havipaswi kuguswa,’’ anaongeza Dkt Adams. ‘’Kwa hiyo wanaleta wazi mbele ya hadhira kile ambacho hakuna anayejua. Hawapaswi kuonekana kuegemea upande wowote au kuwa na maoni ya kibinafsi.’’
Kwa bahati mbaya kuhusu migogoro, sababu na athari zinaweza kutofautiana lakini picha zinafanana.
Vita ni vita. Njaa inaonekana kama njaa kila mahali. Na hii kwa mujibu wa Hassan inakuwa changamoto kuendeleza taarifa kwa muda mrefu.
Uchovu unachangia
‘’Lazima tubuni mbinu mpya za kusimulia taarifa zetu, la sivyo baada ya muda hata watazamaji wetu watachoka.’’ Anaiambia TRT Afrika. ‘’Tuna changamoto ya kuwafanya watu wapendezwe na ripoti la sivyo wataanza kutafuta habari zingine.’’ Anaongeza.
Inasikitisha lakini ndio ukweli wa mambo.
Kamera na maikrofoni hufuata habari za hivi punde. Lakini wataalam wa usalama wanaonya kuwa kupoteza mvuto au hamu ya vyombo vya habari kunaweza kuwa na madhara mashinani.
‘’Ni muhimu kuendeleza taarifa hizi kwa ajili ya watu walio katika mazingira magumu wanaopitia hali ngumu. Hasa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu,’’ anasema Dk Adams. ‘’Lakini usipoangazia kinachoendelea, wale wanaonufaika na mzozo huo wanapata pasi ya bure.’’
Kulingana na Dk Adams, Vyombo vya habari vinaweza kupoteza hamu ya kuripoti mkasa kutokana na kushawishiwa kisha wameridhika na kile kinachotokea kwa hivyo wanaua hadithi. Anasema pia Vyombo vya habari vinaweza kupoteza hamu kwa sababu wamechoka.
‘’Huwezi kuwa unaripoti juu ya jambo moja tena na tena. Mfano, tunayo hali hiyo Kaskazini mwa Ghana ambako kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu.’’ Anasema Dk Adams. Mambo mengi mabaya yanafanyika, mauaji, kuchomwa moto na kutekwa nyara. Lakini vyombo vya habari kwa sasa havina hamu tena kufuatilia.’’
Lakini wakati mwingine vyombo vya habari vinaweza kuendeleza hadithi wakati kuna Maslahi maalum na vikundi fulani vyenye ushawishi.
‘’Nafikiri mizozo barani Afrika inashughulikiwa tofauti kuliko mizozo mahali pengine,’’ asema mwandishi wa habari wa video Hassan.
‘’Unaona, baada ya kukaa majuma machache Sudan, ilinibidi nirudi kwenye habari zingine nyumbani. Lakini ukitazama vita vya Urusi na Ukraine, shirika langu limetuma kikosi cha kudumu huko, inayowasilisha ripoti kila siku. Sidhani wataondoka hadi waone mwisho wa mgogoro huko.’’
Iwe ni vita au njaa au habari nyingine yoyote mbaya, vyombo vya habari huunganisha watu walioathirika na mashirika muhimu ambayo hutoa msaada.
Lakini hii pia inamaanisha, wakati vyombo vya habari vinapoondoka, kuna uwezekano wa maslahi ya kimataifa kupungua pia.
‘’Unapokuwa na mashirika makubwa ya vyombo vya habari yanayoangazia mauaji ya halaiki au mauaji fulani basi utakuwa na wasaidizi wakubwa wanaoingilia kati.’’ Asema Mtaalamu wa Usalama Dkt Adams.
‘’Kwa sababu Umoja wa Mataifa, au mashirika mengine kama EU, AU, ECOWAS na mengine, hawataki kulaumiwa kwamba hawafanyi lolote, hivyo wanaanza kukusanya rasilimali. Kwa hiyo kukikosekana msururu wa hadithi zinazofikia shirika kama UN, basi wanapoteza ile dharura na wanaanza kufuatilia mambo mengine.’’ Anaongeza.
Ni siku 100 pekee tangu mzozo wa Sudan kuzuka. Hassan ambaye alikuwa miongoni mwa wanahabari wa kwanza wa kimataifa kufika huko kuripoti tangu wakati huo amehamia kuandika habari nyingine ikiwa ni pamoja na tamasha la muziki nchini Kenya.
Lakini wapokezi wa habari pia wameanza kutafuta kitu kingine cha kutazama au kusoma. Swali ni je, kelele za Sudan zikififia, je dunia bado itajali kinachoendelea nchini humo na maeneo mengine?