Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Kusini, chama tawala cha ANC kimeshindwa kupata asilimia zaidi ya 50 ya kura./Picha:Reuters  

Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC) imesema kuwa itaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa Mei 29 kuanzia saa 12 jioni, siku ya Jumapili.

Huku kukiwa na zaidi ya asilimia 99 za kura zilizopigwa, chama tawala cha ANC, kimeambulia asilimia 40.2 ya kura zote, hii ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya chama hicho.

Chama cha upinzani cha Democratic Alliance kinashika nafasi ya pili kikiwa na asilimia 21.8, kikifuatiwa na chama cha Rais wa zamani Jacob Zuma, cha uMkhonto weSizwe, kikiwa na asilimia 14.6 ya kura zote.

Zuma apinga matokeo

Zuma ametoa wito wa kuahirishwa kwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, akibainisha kuwa kuna migogoro ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kati mji wa Midrand ulioko katika jimbo la Gauteng siku ya Jumamosi, Zuma alisema: "Tunahitaji muda zaidi (kwa ajili ya kushughulikiwa kwa malalamiko yetu), mtu yeyote asitangaze matokeo siku ya kesho (Jumapili). Natumai wanasikia hili. Wasianzishe vurugu mahali palipotulia."

Zuma pia anadai kwamba kumekuwepo wizi wa kura kwa kukipendelea chama cha ANC.

Maafisa wa chama chake wanadai kuwa makosa hayo ni pamoja na kuingiliwa na mfumo wa Teknolojia ya Habari wa IEC wakati wa hitilafu za kiufundi siku ya Jumamosi.

IEC yathibitisha pingamizi la matokeo ya uchaguzi

IEC ilisema imepokea jumla ya mapingamizi 579 ya matokeo ya uchaguzi kutoka kwa wapiga kura na vyama vya kisiasa, na kuongeza kuwa itashughulikia malalamiko yote kabla ya kutangazwa kwa matokeo siku ya Jumapili.

ANC italazimika kuingia katika mpango wa muungano na vyama vingine, ikizingatiwa kwamba katiba ya Afrika Kusini inadai kuwa chama lazima kiwe na angalau asilimia 50 ya viti vya ubunge ili kuunda serikali peke yake.

Kuna viti 400 katika Bunge la Kitaifa la Afrika Kusini. Ili mgombeaji urais atangazwe kuwa mshindi, ni lazima apate angalau kura 201 za ubunge.

Uchaguzi wa rais, ambao umewahusisha Cyril Ramaphosa wa ANC na John Steenhuisen wa DA, utafanyika ndani ya mwezi mmoja baada ya kutangazwa kwa matokeo rasmi na IEC.

TRT Afrika