Timu ya Taifa ya Wanawake ya Burundi imesonga mbele katika mbio za kuwania kufuzu WAFCON.

Na Ramadhan Kibuga

Timu ya Taifa ya Wanawake ya Burundi imesonga mbele katika mbio za kuwania kufuzu WAFCON, Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake. Burundi wameitoa Ethiopia kwa penati 5-3. Hii ni baada ya mchezo kumalizika timu hizi mbili zikienda sare ya bao moja kama ilivyokuwa katika mechi awali na ndipo mikwaju ya penati ikatumika kutafuta Mshindi.

"Intamba mu Rugamba" ya wanawake walilazimika kucheza mechi zote 2 mjini Addis Abeba kutokana na ukosefu wa uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kukidhi vigezo vya CAF.

"Tunakwenda kufanya maandalizi ya ziada tulifahamu uzito wa mpinzani. Ni kweli Algeria wamepiga hatua katika soka. Lakini kwenye ngazi hii lolote linawezekana."

Kocha Belyze Nininahazwe

Mwalimu msaidizi wa Burundi Bi Belyze Nininahazwe amesema, " Kazi haikuwa rahisi. Kwanza kwa kucheza mechi zote mbili tukiwa nyumbani kwa wapinzani wetu. Lakini tuliwaanda wasichana wetu kichwani kwamba hiyo isiwe hoja na kwamba tunaweza kuwashinda. Unavyojua mechi kama hizi zinaamuliwa na mambo madogo. Lakini tumepambana hadi mwisho. Tulipata nafasi nyingi nzuri pengine hatungekwenda hata kwenye penati."

Burundi itakutana sasa na Algeria katika hatua ijayo baada ya Algeria kuibandua Uganda. Kocha Belyze Nininahazwe anasema hawatetereki kukutana na Algeria: "Tunakwenda kufanya maandalizi ya ziada tulifahamu uzito wa mpinzani. Ni kweli Algeria wamepiga hatua katika soka. Lakini kwenye ngazi hii lolote linawezekana."

"Sasa na sisi tuna wachezaji wetu ambao wamezowea sana mechi za kimataifa. Umecheza WAFCON mwaka jana, sasa tayari tumeshaonja na hii itatusaidia kuwa na hamasa maana wengi waliocheza lile shindano wamo kwenye kikosi chetu. Isitoshe wengi mwa hao wanacheza sasa ligi ngumu kama Tanzania, Uganda na Misri. Tunaamini wasichana wetu watapambana vya kutosha dhidi ya Algeria na kurudi tena kwenye mashindano hayo. Tutaomba tu mechi za maandalizi za kutosha."

Burundi ilifuzu na kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya kombe la mataifa Afrika kwa wanawake WAFCON mwaka uliopita nchini Morocco.

Lakini licha ya mafaaniko hayo Burundi imo katika nafasi ya 175 kwa ujumla ya Mataifa 186 kwenye viwango vya ubora wa soka kwa wanawake vinavyochapishwa na FIFA.

TRT Afrika