Na Suleiman Jongo
TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania
Ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania kwa ajili ya mechi ya African Super League kati ya Simba Sports Club na Al-Ahly ya Misri utakamilika Oktoba 10, Waziri wa Michezo nchini humo Dk. Damas Ndumbaro amesema.
Simba itacheza na vigogo hao wa Afrika, Al-Ahly katika hatua ya Robo Fainali Oktoba 20, 2023 na marudiano ya mechi hiyo itakuwa Cairo, Misri Oktoba 24, 2023.
Michuano hii iliyoanzishwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ni mipya barani Afrika ambapo kwa sasa itashirikisha timu nane, huku Simba ikiwa ndio timu pekee kutoka nchini Tanzania.
Akitoa ripoti ya maendeleo ya ukarabati wa uwanja huo kwa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Waziri Dk. Ndumbaro amesema sehemu kubwa ya ukarabati wa uwanja kwa ajili ya mechi hii kubwa inayosubiriwa kwa hamu imekamilika, huku akisema kuwa ukarabati wa uwanja huo bado unaendelea kwa ajili ya fainali za AFCON mwaka 2027 ambapo Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja watakuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka duniani.
Waziri Mkuu Majaliwa ameonyeshwa kuridhishwa na ukarabati huo, ambao umehusisha maeneo mbalimbali ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo za wachezaji, chumba maalum cha kupimia afya za wachezaji na vyumba vya matangazo.
Akiongea wakati alipotembelea uwanja huo wakati wa kukabidhi milioni 500 zilizotolewa na Rais Samia kwa kuwapongeza Stars kufuzu AFCON 2023, Waziri Mkuu amesema serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuwekeza vilivyo katika sekta ya michezo.
“Uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.”amesema.
Serikali ya Tanzania ilitenga takriban bilioni 31 kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo mkubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kwa ajili ya michuano ya AFCON.
Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu elfu sitini wakiwa wamekaa, ulijengwa wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjami William Mkapa zaidi ya miongo miwili iliyopita kwa gharama zinazokadiriwa kuwa takriban bilioni 60.
Ukiachia mbali Simba na Al-Ahly, timu nyingine zitakazoshiriki michuano hii ya African Super League ni Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini, Waydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya watu wa Kongo [ DRC), Petro Atletico ya Angola na Enyimba ya Nigeria.