Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Wadau wa utalii nchini Tanzania wana mategemeo na soko la Uturuki kama njia mojawapo ya kukuza na kupanua wigo wa biashara hiyo.
Watu hao muhimu katika sekta hiyo inayoihakikishia Tanzania kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 2 kila mwaka, wanaielezea nchi ya Uturuki kama soko la uhakika na la kimkakati katika kufikia malengo iliyojiwekea ya kupokea watalii milioni 5, ifikapo mwaka 2025.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO) Sirili Akko, anaiambia TRT Afrika kuwa Uturuki ni soko muhimu lenye uwezo wa kuihakikishia nchi ya Tanzania watalii wengi zaidi, katika siku zijazo.
Kulingana na Akko, sababu zinazoifanya Uturuki kuwa soko tegemeo katika kukuza biashara ya utalii nchini Tanzania ni uwepo kwa usafiri wa ndege za moja kwa moja kutoka Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi Istanbul na idadi kubwa ya Watanzania wanaosafiri kwenda Uturuki kwa ajili ya huduma bora za afya.
“Uturuki imeonesha nia thabiti ya kuwekeza kwenye sekta ya ujenzi nchini Tanzania, na sisi kama wadau wa utalii, tutahakikisha tunaitumia fursa hiyo kikamilifu," Akko anaeleza.
Kama ishara ya kutambua umuhimu wa Uturuki katika kukuza biashara ya utalii Tanzania, ujumbe wa TATO uliitembelea nchi hiyo Novemba 2023 na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki.
Hatua hii inakuja wakati ambapo jumla ya watalii 655 kutoka Uturuki, wamekwisha zitembelea baadhi ya hifadhi za Taifa nchini Tanzania, kati ya mwezi Julai na Disemba 2023.
Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) zaidi ya watalii 4,000 kutoka Uturuki wametembelea hifadhi zake, kati ya kipindi kinachoanzia Julai 2018 mpaka Disemba 2023.
“Hii ni habari njema na kubwa kwetu kama mawakala wa utalii kwani itatufanya tuendelee kushirikiana na Uturuki katika kufikia malengo yetu,” Akko aliongeza.