Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, January Makamba akiwa na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan./Picha: JMakamba X.

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Ziara ya kikazi ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania nchini Uturuki, inalenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili, amesema January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.

Makamba, ambaye alikutana na mwenyeji wake, Hakan Fidan ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Aprili 16 jijini Ankara, amebainisha kuwa Tanzania inategemea kusaini mikataba minane na Uturuki, kama sehemu ya kukuza uhusiano na kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Makamba, Rais Samia analenga kutumia ziara hiyo ya kiserikali kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania.

"Uturuki ni chanzo muhimu cha uwekezaji na mapato ya nje. Ziara hii inalenga kuimarisha hili," amendika Makamba kupitia ukurasa wake wa X.

Wakati wa ziara yake, Rais Samia anatarajiwa kukutana na wafanyabiashara wakubwa 100 kutoka Uturuki, kwa nia ya kuwahamasisha kuwekeza nchini Tanzania.

Makamba aliongeza kuwa makubaliano kati ya nchi hizo mbili yataangazia maeneo mbali mbali ikiwemo, elimu ya juu, teknolojia na ubunifu.

"Makubaliano sita yamekwishapitishwa, kuna uwezekano wa kuwepo na mengine," amedokeza.

Kulingana na Makamba, Uturuki ni kati ya nchi za G20 duniani, zenye fursa lukuki za kuwekeza Tanzania, kwa ajili wa ustawi wa kijamii na kiuchumi wa nchi hizo mbili.

Akiwa nchini Uturuki, Rais Samia, pia anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake, Rais Recep Tayyip Erdoğan.

Ziara hiyo ya kikazi inakuja miaka 14 toka Rais wa Tanzania kuitembelea Uturuki, wakati Rais Erdoğan aliitembelea Tanzania mwaka 2017.

TRT Afrika