Takriban watu 44 wameuawa katika mji mkuu wa Kordofan Kusini, Kadugli. /Picha: AP / Photo: AA Archive

Takriban raia 44 wameuawa na wengine 28 kujeruhiwa katika shambulio lililotekelezwa na kikundi cha Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N) kinachoongozwa na Abdelaziz al-Hilu huko Kadugli, mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kusini, kusini mwa Sudan, mamlaka ilitangaza Jumatatu.

SPLM-N imekuwa ikipambana na jeshi la Sudan huko Kordofan Kusini na Blue Nile tangu 2011, wakidai hadhi maalum kwa mikoa hiyo miwili.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Sudan, vikosi vya SPLM-N vilishambulia Kadugli kwa makombora Jumatatu asubuhi, na kusababisha madhara makubwa, miongoni mwa waliouawa, ni wanawake na watoto. Imam Nizar Mohamed Tom, Imamu katika Msikiti wa Kihistoria wa Kadugli ni miongoni mwa waliouawa.

Gavana wa Kordofan Kusini Mohamed Ibrahim Abdel Karim amelaani shambulizi hilo na kulitaja kama "uchokozi wa dhidi ya raia."

Alisema jeshi la Sudan limekabiliana na hali hiyo kama inavyotakiwa, na kuwasababishia hasara kubwa waasi hao, wakiwemo wafanyakazi, magari na vifaa, huku pia wakikamata silaha na risasi.

Kamanda wa jeshi la Sudan Faisal Mukhtar wa Kitengo cha 14 cha Wanajeshi alisema kuwa vikosi vya jeshi vimedhibiti tena eneo la Kadugli. SPLM-N bado haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo.

Matukio hayo ya Kordofan Kusini yanatokea wakati jeshi la Sudan likiendeleza udhibiti wake katika majimbo ya Khartoum na Al Jazirah, ambapo limekuwa katika mapigano na Vikosi vya RSF tangu Aprili 2023.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na wengine karibu milioni 14 wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na Mamlaka ya Sudan. Lakini, utafiti kutoka chuo kikuu cha Amerika unasema idadi ya vifo inaweza kuwa 130,000.

Mashirika ya kimataifa yanaendelea kuonya juu ya janga baya kwa watu linalokaribia wakati mapigano yameenea hadi majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan, na kusababisha njaa kwa mamilioni ya watu na wengine kufa kutokana na uhaba wa chakula.

AA