Idadi ya vifo vinavyotokana na mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan imeongezeka hadi kufikia 348, hiyo ni kulingana na Wizara ya Afya.
Mlipuko huo umeathiri majimbo tisa, na zaidi ya wagonjwa 11,000 wameripotiwa. Wakati huo huo, kuna wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka kwa homa ya dengue, baada ya vifo viwili vinavyoshukiwa.
Mvua kubwa na mafuriko yamezidisha kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu tangu Juni. Kudorora kwa mfumo wa huduma ya afya nchini Sudan kumefanya juhudi za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kuwa ngumu zaidi.
Janga kubwa
Waziri wa Afya wa Sudan Haitham Ibrahim mwezi Agosti alitangaza janga la kipindupindu baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa katika nchi hiyo.
Haitham Ibrahim alisema uamuzi huo umechukuliwa kwa kushirikiana na mamlaka katika jimbo la mashariki la Kassala, mashirika ya Umoja wa Mataifa, na wataalamu baada ya "kugunduliwa na maabara ya afya ya umma ya virusi vya kipindupindu."
Nchi hiyo ya kaskazini-mashariki mwa Afrika imekumbwa na vita tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan chini ya mtawala mkuu wa nchi hiyo Abdel Fattah al-Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), kinachoongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.
Mgogoro huo umeibua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni 25 -zaidi ya nusu ya idadi ya raia wa Sudan - wakikabiliwa na njaa kali.
Uhaba wa chakula
Njaa imetangazwa katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo kubwa la magharibi la Darfur.
Maelfu ya watu wameyahama makazi yao kutokana na mafuriko na kusababisha ongezeko la magonjwa ikiwemo kuharisha hasa kwa watoto.
Kipindupindu husababisha hali ya kuharisha, kutapika, na kukakamaa kwa misuli, na kwa ujumla hutokana na kula au kunywa chakula au maji ambayo yamechafuliwa na bakteria, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Inaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini, na kusababisha katika hali zingine kifo ndani ya masaa machache.