Kiongozi wa mpito wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan/ Picha: AFP

Utawala wa Sudan umekaribisha maazimio ya mataifa jirani yanayolenga kukomesha mzozo unaoendelea nchini humo.

Nchi jirani za Sudan, zilizokutana mjini Cairo, Misri siku ya Alhamisi, zilipendekeza kufanikishwa kwa mazungumzo ya kitaifa na ya kina yenye kujumuisha wahusika wote wa Sudan na kuanzisha utaratibu wa mawaziri wa kusitisha mapigano yanayoendelea.

Likizungumzia maafikiano ya mkutano huo wa majirani, Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan, linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan, lilisema: "Serikali ya Sudan inakaribisha matokeo ya mkutano wa kilele wa nchi jirani za Sudan... Pia tunatoa shukrani zetu kwa nchi jirani za Sudan zilizoeleza misimamo inayounga mkono usalama na utulivu wa Sudan.”

Baraza hilo lilizidi kusema "Majirani wamethibitisha nia yao ya kufanya kazi na pande zote zinazotaka kusitisha mapigano na kurejesha usalama na utulivu katika nchi yetu tuipendayo."

Wakati huo huo Naibu Mwenyekiti wa Baraza kuu la utawala nchini Sudan Malik Agar amekaribisha juhudi na mipango ya upatanishi inayoendeshwa na majirani wa Sudan na wahusika wengine wakiwemo IGAD, na AU. Alisema hayo baada ya kukutana na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa huko Johannesburg, Afrika Kusini.

TRT Afrika