Asasi za kisiasa na kiraia Sudan zimekubaliana kuunda shirika la uongozi wa maandalizi ya muungano mmoja wa kidemokrasia wa kiraia wa kumaliza vita Sudan.
Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan Abdalla Hamdok ameteuliwa kusimamia maandalizi ya mkutano wa uanzilishi uliopangwa kufanyika ndani ya muda wa wiki nane.
Haya yalijiri baada ya wawakilishi wapatao mia moja wa makundi ya kisiasa, asasi za kiraia, na makundi mengine ya kijeshi kukutana Addis Ababa, Ethiopia kuunganisha vyama vinavyosaka kurejeshwa kwa utawala wa mpito wa kiraia wa kidemokrasia nchini Sudan.
Makundi ya kisiasa na ya kiraia ya Sudan, yalikutana kwa siku tatu kutoka Oktoba 23 hadi 26, na kuafikiana juu ya muundo wa shirika, pamoja na chombo cha uongozi cha "Uratibu wa vikosi vya Kidemokrasia vya kiraia" (CCDF) kilicho na wawakilishi 60 kut vikosi vya kisiasa na vya kiraia, pamoja na ofisi ya utendaji iliyo na wanachama 30 ili kujiandaa kwa mkutano wa kwanza wa uratibu.
Aidha, kamati hiyo inayoongozwa na Abdalla Hamdok, ilikaribisha kurejea tena kwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili zinazopigana, kwenye mazungumzo ya amani mjini Jeddah na kuthamini juhudi za Saudi arabia na Marekani.
Hamdok aliyashukuru mataifa jirani na jumuiya ya kikanda na kimataifa kwa msaada wao na kuwaomba kukomesha vita na kushughulikia mgogoro wa kibinadamu.
Vile vile, aliisifu Saudi arabia, Marekani, Mamlaka ya Serikali za Maendeleo (IGAD), na Umoja wa Afrika (AU) katika juhudi zao za kukomesha vita nchini humo.
Nchi za Troika (Norway, Uingereza, na Marekani) zilipongeza mkutano huo wa makundi ya kiraia ya Sudan wakisema kuwa ni hatua muhimu kuelekea kuundwa kwa umoja na uwakilishi wa demokrasia ya raia.