Na
Edgar Githua
Sudan imekuwa katika mzozo mkali kwa zaidi ya mwaka mmoja. Makundi mawili hasimu ya kijeshi ambayo hapo awali yalifanya kazi pamoja yalianza kupigania mamlaka mnamo 2023 na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kikosi cha Jeshi la Sudan (SAF) chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na kundi la RSF chini ya kiongozi wa zamani wa Janjaweed, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, wamezozana na kusababisha mzozo ulioanza tarehe 15 Aprili 2023.
Kiini cha mzozo huo kilikuwa ni kuanguka kwa mpango wa kugawanya madaraka kati ya Jenerali al-Burhan na Jenerali Dagalo. Wawili hawa wamefanya kazi pamoja katika kumwondoa madarakani aliyekuwa Rais Omar al Bashir mwaka wa 2019.
Chanzo kikuu cha mzozo kilikuwa ni muungano uliopangwa wa kikosi cha SAF na RSF chini ya kiongozi mmoja. Hasa, RSF ilitarajiwa kuvunjwa na kuunganishwa na jeshi kuu la Sudan, hatua ambayo Dagalo hakupendela itekelezwe kutokana na hofu ya kupoteza mamlaka.
Baada ya kuvunja serikali ya kiraia mwaka wa 2021, Burhan na Dagalo hawakuonekana kuweza kufanya kazi pamoja na hatimaye mzozo ukazuka. Mgogoro huo katika mwaka mmoja uliopita umesababisha vifo vya takriban watu elfu kumi na nne, na wengine mamilioni wamehama makazi yao.
Usitishaji mapigano umeshindwa
Kumekuwa na majaribio mengi ya kurejesha amani nchini Sudan. Hata hivyo, majaribio haya yameshindwa kuzaa matunda, kutokana na maslahi mengi yanayoshindana katika siasa za kikanda, na kimataifa.
Kushindana kwa maslahi ya kigeni imechangia kukosekana suluhu na amani. Kiini cha mashindano haya ni hitaji la kudhibiti au kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Sudan kutokana na nafasi yake ya kimkakati barani Afrika.
Iran na Urusi zinaiona Sudan kama njia ya kuzindua ushawishi wao katika bara la Afrika, na zimekuwa zikimshawishi Jenerali Burhan kuwaruhusu kujenga vituo vya jeshi la majini kwenye Bahari Nyekundu.
Michakato kadhaa ya kuleta amani imeanzishwa na jitihada za kumaliza mzozo nchini Sudan. Ikiongozwa na Marekani, Saudi Arabia na IGAD, mikataba iliyotiwa saini imekiukwa huku pande zote mbili zikiendelea na harakati za kijeshi.
Ukosefu huu wa amani unaweza kuchangiwa na kutokuwa na nia njema juu ya uongozi wa pande zinazozozana katika mgogoro huo.
Athari za vita
Mzozo wa Sudan umezua mgogoro mkubwa na hali mbyaya ya kibinadamu katika nchi na eneo hilo. Hii imesababisha watu kuhama makazi yao, uhaba wa chakula na ukosefu wa huduma za msingi.
Mgogoro wa wakimbizi katika eneo hilo pia umeendelea. Takriban watu milioni nane ni wakimbizi wa ndani, wanaishi katika hali mbaya, bila vyoo na huduma nyingine muhimu.
Watu wengine wanaokadiriwa kufikia milioni mbili wameikimbia nchi hiyo na kwa sasa wako Chad, Sudan Kusini, Libya na Misri, na hivyo kusababisha mgogoro mwingine wa kijamii na kiuchumi katika nchi hizo.
Uhaba wa chakula ni mzozo mwingine mkubwa unaoikabili Sudan na mzozo unaokumba chanzo cha chakula nchini humo katika jimbo la Al Jazirah.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linaripoti kuwa takriban watu milioni 18 nchini Sudan wanakabiliwa na njaa.
Tatizo hilo linachangiwa na ukame katika nchi jirani ya Sudan Kusini, na Chad ambako wakimbizi wengi wa Sudan wametafuta hifadhi.
Hali imekuwa mbaya, huku mashirika ya misaada yakiomba msaada kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Mgogoro unaoendelea nchini Sudan umekuwa na sifa ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya raia, unyanyasaji wa kijinsia, na kufurushwa.
Wapiganaji hao wa RSF na SAF wameshutumiwa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na Umoja wa Mataifa kwa kufanya ukatili, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa uhalifu mkubwa wa kivita na mauaji ya kusudi. Hii inatoa picha mbaya sana ya mzozo unaoendelea.
Suluhu ni ipi
Mzozo wa Sudan umekuwa mgumu kutokana na kuwepo kwa wahusika wa nje wenye maslahi katika eneo hilo. Maslahi ya Urusi katika biashara ya dhahabu nchini Sudan pamoja na mahusiano ya kibiashara na Jenerali Dagalo yamechochea mzozo huo.
Jenerali Khalifa Haftar kutoka Libya pia amedaiwa kumuunga mkono Dagalo zaidi. Kwa upande mwingine, Misri inadaiwa kumuunga mkono Jenerali Burhan.
Ili kupatikana amani nchini Sudan, jumuiya ya kimataifa inahitaji kuwawekea vikwazo wahusika wa nje ambao wamekuwa wakitoa msaada kwa makundi haya mawili.
Kujiondoa kwa wahusika wa nje kutawahimiza wahusika wakuu kukaa chini na kupanga njia ya kusonga mbele. Hili linapaswa kufuatiwa na juhudi za pamoja za kidiplomasia ili kuwafanya wahusika wakuu kumaliza mzozo huo.
Jumuiya ya Kimataifa pia inahitaji kufanya zaidi kusaidia kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu ambao umekuwa ukiendelea nchini humo.
Msaada zaidi unahitaji kupelekwa kwa jamii na kanda zilizoathirika sio tu ndani ya Sudan lakini katika eneo zima.
Msaada wa chakula kwa wakati, dawa na huduma zingine za kimsingi zinapaswa kupelekwa kwa watu walioathiriwa, sio tu kwa lengo la kuhifadhi utu wao bali pia kuokoa maisha.
Mwandishi, Dkt. Edgar Githua, ni mtafiti wa mahusiano ya kimataifa, amani na migogoro, na mchambuzi wa usalama katika Chuo Kikuu cha Strathmore nchini Kenya.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi maoni, maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.