Aprili 15 2023, dunia iliamkia taarifa za milio ya risasi na milipuko ya bomu katika mji mkuu wa Sudan Khartoum, na muda mfupi baadaye rabsha zikaenea katika miji mingine.
Taarifa zikaenea kuwa wapiganaji wa kikosi cha dharura RSF, wamedai kuteka kasri ya rais, kambi za kijeshi na kuvamia na kuteka kituo cha televisheni ya taifa mjini Omdurman.
Kilichofuatia, ufyatulianaji wa risasi na kulipua mabomu kati ya jeshi la taifa na wapiganaji wa RSF, na mwaka mmoja baadaye, bado milipuko inarindima nchini humo licha ya maelfu kuuawa n amamilioni kukimbia nchi, huku dalili zikionekana za kutokea uhalifu wa kivita wa hali ya juu.
Basi hawa wanaopigana nchini Sudan ni kina nani?
Vita nchini Sudan ni kati ya Jeshi la Taifa na RSF. Tuwamulike kwa undani zaidi.
Jeshi la Taifa
Vikosi vya kijeshi vya Sudan, vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, vilikuwa katika nafasi bora zaidi mwanzoni mwa vita kwa sababu ya idadi kubwa ya wanajeshi, silaha zao nzito na ndege za kivita.
Ni taasisi iliyokuwa katika kitovu cha mamlaka nchini Sudan kwa miongo kadhaa. Burhan - aliyezaliwa mwaka 1960 katika kijiji kaskazini mwa Khartoum jirani na nyumbani kwa Bashir - ametumikia maisha yake yote katikati mwa taasisi hiyo.
Hata hivyo, kumbuka jeshi hilo la taifa katika miaka ya nyuma mara nyingi walitoa kandarasi ya kushiriki makabiliano na waasi hasa katika eneo la Kusini Magharibi la Darfur kwa makundi washirika katika mikoa mbalimbali ya Sudan – ikiwa ni pamoja na wanamgambo ambao baadaye walikuja kujiita RSF.
Chini ya Uongozi wa Bashir, Burhan alihudumu huko Darfur, ambapo serikali ilipigana kukomesha uasi katika ghasia ambazo zilisababisha takriban watu milioni 2 kuyahama makazi yao na vifo zaidi ya 300,000 kufikia mwaka 2008. Pia alianzisha uhusiano na mataifa ya Kiarabu, na kusaidia kusambaza wanajeshi kwa Saudi- ambao walitumika katika mapigano nchini Yemen.
Burhan anajisifia kuwa miongoni mwa viongozi wa kijeshi waliomshinikiza Bashir kuachia ngazi, na kuibuka haraka baadaye kama kiongozi madhubuti wa Sudan.
Japo miezi kadhaa ya vita, RSF iliweza kunyakua sehemu nyingi za kijeshi eneo la Khartoum na Darfurna jimbo la Al Gezira, mwanzoni mwa mwaka huu jeshi la taifa limekuwa likikomboa miji hiyo moja baada ya nyingine.
Jeshi hilo linadaiwa kupokea uungwaji mkono kutoka kwa mataifa ya kigeni ikiwa ni pamoja na nchi jirani ya Misri na kwa kiasi kikubwa inashikilia Sudan kaskazini na Mashariki ikiwa ni pamoja na Bandari ya Sudan kwenye Bahari Nyekundu.
RSF
RSF inaongozwa na tajiri mkubwa ambaye wakati mmoja alikuwa kiongozi wa wanamgambo, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu zaidi kama Hemedti.
Wachambuzi walikadiria kuwa kikosi hicho kilifikia 100,000 kabla ya vita kuanza, waliosambazwa kwa vituo mbali mbali kote nchini.
Hemedti, ambaye anaaminiwa hakumaliza masomo yake ya shule sasa akiwa katika miaka yake ya mwisho ya 40, alianza kama mfanyabiashara wa ngamia huko Darfur.
Kulingana na Muhammad Saad, msaidizi wake wa zamani, Hemedti alichukua silaha kwa mara ya kwanza baada ya watu kushambulia msafara wake wa wafanyabiashara, kuua takriban watu 60 kutoka kwa familia yake na kuiba mifugo yake.
Ustadi wake wa kupigana uliimarishwa wakati wafuasi wake na waasi wengine waliposhirikiana na serikali kusaidia kukomesha uasi huko Darfur katika kampeni ambayo iliongezeka mwaka wa 2003.
Vikosi vya wanamgambo vilijulikana kama Janjaweed, jina la kiarabu lililoashiria 'mashetani walioko juu ya farasi' ambalo lilionyesha sifa yao ya kutisha.
Japo Hemedti mwenyewe hakutajwa kwa jina, kundi hilo la Janjaweed lilishutumiwa kimataifa kwa mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita.
Baada ya muda RSF katika mwaka 2017 ilipata kutambuliwa rasmi kama kikosi cha kijeshi kwa msaada wa Bashir, lakini huku pembeni maslahi ya kibiashara ya Hemedti yalitanuka katika uchimbaji wa dhahabu, ujenzi, mifugo na maeneo mengine.
Vikosi vya RSF vimetambuliwa kuwa adui wa kijanja vitani, wakiteka baadhi ya vituo vyao na kjificha katika maeneo ya makazi ambapo silaha nzito na mbinu za kijeshi za kawaida hushindwa kutumika.
Mshirika muhimu zaidi wa Hemedti imekuwa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, kwa mujinbu wa vyanzo vya Sudan na wachambuzi na wanadiplomasia japo UAE imekanusha ripoti za kutuma shehena za silaha kwa RSF.