Mamlaka ya Mawasiliano ya Sudan Kusini imepiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari 22, 2025.
Katika tangazo lake kwa watoa huduma za intaneti lililotolewa Januari 22, 2025 mamlaka hiyo imesema kuwa, katazo hilo linafuatia kusambaa kwa picha za video zinazoonesha mateso na masumbuko ya wakimbizi wa Sudan Kusini walioko katika eneo la Wad Medani, nchi jirani ya Sudan
Kulingana na mamlaka hiyo, maudhui hayo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za Sudan Kusini na pia yanaweza kuhatarisha usalama wa umma.
“Kwa kurejea kifungu namba 9(g) (f) na namba 34(6) cha Sheria ya Mawasiliano ya mwaka 2012, watoa huduma wote wanaagizwa kusitisha utoaji wa huduma za mitandao ya kijamii kuanzia saa 6 usiku ya Januari 22, 2025 kwa kipindi cha siku 90,” ilisema mamlaka hiyo.
Kulingana na mamlaka hiyo, picha hizo zilionesha vifo vya watoto na akina mama na kusambazwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii bila kujali madhara yake.
“Tunaomba tusitishe huduma hii kwa kipindi hicho. Hata hivyo, katazo hili linaweza kuondolewa mara tu hali itakapodhibitiwa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mamlaka ya Mawasiliano ya nchi hiyo ilisisitiza kuwa maudhui hayo yaliyosambazwa yanaweza kuhatarisha usalama wa nchi na madhara ya afya ya akili hasa kwa raia wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.