Shirika la madaktari la MSF linasema zaidi ya watu 5,000 wamevuka hadi Sudan Kusini kila siku tangu mwanzoni mwa Disemba 2024/ Picha: NRC

Zaidi ya watu 5,000 wamevuka hadi Sudan Kusini kila siku tangu mwanzoni mwa mwezi Disemba, wakati mapigano yakiongezeka karibu na mpaka katika majimbo ya White Nile ya Sudan, Blue Nile na Sennar, Shirika la Kibinadamu la Madaktari la MSF limesema katika taarifa mpya.

Vita nchini Sudan vimekuwepo tangu Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Response Forces, RSF.

MSF inasema kumiminika kwa watu katika mji wa Renk na maeneo ya jirani kumefanya rasilimali ambazo tayari zimeadimika kuzidiwa, na kuwaacha watu waliokimbia makazi yao katika mgogoro.

"Tumeongeza mahema 14 kuzunguka hospitali ili kutoa nafasi kwa ajili ya wagonjwa walioathiriwa na vita, na waliojeruhiwa ambao wanawasili katika Hospitali ya Kaunti ya Renk," anasema Emanuele Montobbio, mratibu wa dharura wa MSF huko Renk.

"Tunafanya kazi pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kutibu wagonjwa waliojeruhiwa katika vita na kudhibiti kuongezeka kwa visa muhimu na mwitikio wa majeruhi wengi katika wodi za kabla na baada ya upasuaji, lakini hali ni mbaya sana na uwezo wetu hautoshi," Montobbio ameongezea.

"Kijiji chetu kilikuwa kikiwaka moto," anasema Alhida Hammed, ambaye amefukuzwa kutoka jimbo la Blue Nile nchini Sudan na kwa sasa anaendelea na matibabu ya jeraha la risasi katika Hospitali ya Kaunti ya Renk.

“Nyumba zilikuwa zinawaka moto, na kila mtu alikuwa akikimbia pande tofauti. Tumehamishwa sasa tunaishi chini ya mti. Sina hamu ya kurudi nyumbani. Nyumbani si nyumba tena—imejaa kumbukumbu mbaya." aliambia wahudumu wa MSF.

MSF inasema ni watu wachache tu wametibiwa kwa upasuaji na waliopata chanjo ya pepo punda katika wiki za hivi karibuni, huku zaidi ya wagonjwa 100 waliojeruhiwa, wengi wao wakiwa na majeraha mabaya, bado wanasubiri upasuaji.

Nje ya vituo vya kuwapokea watu ndani ya Renk na katika makazi yasiyo rasmi, maelfu wanalazimika kuishi chini ya miti au katika makazi ya muda, na upatikanaji mdogo wa chakula, maji safi, huduma za afya au huduma nyengine zozote za kimsingi.

Hali duni ya maji na usafi wa mazingira inaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa wakati ambapo Renk tayari inakabiliwa na mlipuko unaoendelea wa kipindupindu.

"Hatua za haraka lazima zichukuliwe," anasema Roselyn Morales, Naibu Mratibu wa matibabu wa MSF nchini Sudan Kusini, kufuatia tathmini ya timu hiyo.

"Vituo viwili vya usafiri vya Renk, vilivyoundwa kuchukua watu wasiozidi 8,000, sasa vinahifadhi zaidi ya 17,000. Wakati wakimbizi wengi waliorejea na wakimbizi waliingia Sudan Kusini kupitia kivuko rasmi cha mpaka cha Joda, idadi inayoongezeka sasa wanavuka kupitia njia zisizo rasmi kuelekea mashariki mwa Renk," Morales amesema.

Zaidi ya wakimbizi wapya 82,000 wapya wamerekodiwa katika maeneo yakiwemo Joda, Duku Duku, Jerbana, Shemmedi, Gosfami na Atam.

TRT Afrika