Serikali ya Sudan Kusini, siku ya Ijumaa imesema itaondoa katazo la matumizi ya mitandao ya kijamii yakiwemo majukwaa ya Facebook na TikTok nchini humo.
Katazo hilo lilifuatia kusambaa kwa picha za video zinazoonesha mateso na masumbuko ya wakimbizi wa Sudan Kusini walioko katika eneo la Wad Medani, nchi jirani ya Sudan.
"Tulikuwa tumewalenga wasambazaji wa picha hizo mbaya," alisema Napoleon Adok, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya taifa ya Mawasiliano nchini humo, huku akigusia kuwa hawakuwa wamelenga “kufungia mitandao yote ya kijamii ".
"Najua kuwa maamuzi hayo hayakupokewa vizuri na umma na tumetilia maanani hoja za raia na vikundi vya haki za binadamu," aliongeza.
TRT Afrika