Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Genetawi Taddesse dereva wa teksi katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa anasema maisha nchini Ethiopia yanazidi kuwa ghali siku baada ya siku.
"Hoteli nyingi za Addis Ababa zimejaa raia kutoka Sudan, wengi wakiwa wamekimbilia nchini kwetu," anaiambia TRT Afrika.
Wafanyabiashara wengi jijini humo, wametumia fursa hiyo kupandisha bei ya bidhaa adimu, kulingana na Taddesse.
"Hii inatupa ugumu sana kama nchi, wakati ambao bado tunakabiliwa na athari za mzozo wa miaka miwili ulioathiri uwezo wetu wa manunuzi na kwa upande mwingine wakimbizi nao wanatuongezea mzigo wa matatizo yetu. Nia yetu ni kuona wanapata amani, kwani hata wale wanaoishi kwenye hoteli kubwa hawana uhakika watakaa hapo kwa muda gani, " anasema.
Zaidi ya Wasudan 90,000 waliokimbia vurugu nchini mwao, wanatafuta hifadhi Ethiopia, ulioanza Aprili 2023 kati ya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Rapid Support Forces, wengi wao wakiwa wanaishi kwenye kambi za wakimbizi.
Hili linakuja wakati idadi kubwa ya Wasudan inatarajiwa kukimbilia Ethiopia kutafuta hifadhi huku jitihada za kutafuta suluhu kati ya Abdel Fattah mkuu wa jeshi la Sudan na mwenzake Mohamed Hamdan Dagalo, kutoka Rapid Support Forces zikigonga mwamba.
Vile vile, Sudan imetangaza uamuzi wake wa kusimamisha uanachama wake ndani ya IGAD.
IGAD, jumuiya inayoundwa na nchi nane zikiwemo Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Eritrea na Uganda, ilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha amani inapatikana nchini humo.
"IGAD ina jukumu muhimu katika upatanishi wa Sudan kwani inaungwa mkono na raia wenyewe wa Sudan na makundi mengine ya kisiasa, na hivyo, uamuzi huu unaweza kuathiri mchakato mzima wa kutafuta amani na hatimaye kucheleweshwa kuanzishwa kwa serikali ya mpito ya kiraia nchini humo, " Nuur Mohamud Sheekh, msemaji wa zamani wa IGAD anaiambia TRT Afrika.
Sudan haina utii kwa IGAD
Kujiondoa kwa Sudan katika jumuiya IGAD kunakuja baada ya Jenerali Abdel Fattah kususia mkutano wa wakuu wa nchi za IGAD uliofanyika nchini Uganda tarehe 18 Januari, akiituhumu jumuiya hiyo kuijumuisha Sudan kwenje ajenda bila kushauriana nayo kabla.
Mualiko wa mpinzani wake, kiongozi wa Rapid Support Forces, Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, kwenye mkutano wa kilele wa IGAD haukupokelewa vyema na kiongozi wa sasa wa Baraza Kuu la Sudan.
Mkutano wa marais wa IGAD ulitoa siku 14 kwa Mejenerali hao kukutana ana kwa ana ili kumaliza uhasama wao.
Hatua hii iliikera serikali ya Sudan.
"Sudan ilisusia mkutano huo, na taarifa zinasema kuwa Sudan ilishushiwa heshima kwenye mkutano huo na kukera familia za waathirika wa machafuko yanayosababishwa na waasi," ilisema serikali ya Sudan katika taarifa yake.
Katika mkutano wao Desemba 2023 wakuu wa nchi za IGAD walihakikishiwa kuwa Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na mwenzake wangekutana kwa mazungumzo ya amani.
"Hata kama Sudan ina wasiwasi na IGAD, uamuzi wa kusimamisha uanachama wake haufai," Sheekh msemaji wa zamani wa IGAD anaiambia TRT Afrika, "Shirika hilo limeweka taratibu za kushughulikia malalamiko kupitia vyombo vyake vya sera, pamoja na wakuu wa Serikali .”
Kuzorota kwa hali za Kibinadamu
Uamuzi wa Sudan kusimamisha uanachama wake IGAD, umeleta hofu ya kuongezeka mapigano zaidi nchini humo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 7.6 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya Sudan tangu mapigano yalipozuka tarehe 15 Aprili 2023.
"Idadi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan imeongezeka kwa takriban 19,600 wiki iliyopita," shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na maswala ya kibinadamu, UNOCHA lilisema tarehe 21 Januari 2024.
"Kwa sasa, Sudan ndiyo nchi inayoongoza kwa watu waliyoyakimbia makazi yao duniani," imeongeza.
Vita hivyo tayari vina madhara kwa majirani wa Sudan.
"Machafuko ya Sudan yamesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu mashariki mwa Chad, ambapo karibu watu milioni moja na nusu wamepata hifadhi, pamoja na jamii ambazo tayari ziko hatarini na maelfu ya wakimbizi wengine wa Sudan ambao wamekuwa nchini kwa miongo miwili," shirika la MSF limesema.
MSF ni shirika la kimataifa, lenye kutoa msaada wa matibabu kwa watu walioathiriwa na migogoro na maafa mengine.
Kwa mujibu wa MSF, ni hospitali chache tu mjini Kartoum zenye kutoa huduma za kitabibu, huku bei ya madawa ikendelea kupanda.
"Wengi hufika hapa wakiwa na hali mbaya wakati mwingine kulazimika kusafiri umbali mrefu kwa miguu ili kukwepa vita kutokana na uhaba wa magari ya kusafirisha wagonjwa," imeongeza MSF.
"Mamilioni ya watu nchini Sudan wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. Lakini ni wachache mno kati yao wanaoipokea kutokana na changamoto za usalama."
Mgogoro huu umeweka ugumu kwa mashirika ya kutoa misaada ya dharura kufikia watu kwa wakati hasa kwenye maeneo yaliyotwaliwa na RSF.
Huku Sudan ikijitenga na IGAD, upatikanaji wa misaada ya kibinadamu unaelekea kuwa mbaya zaidi huku Majenerali hao wakiendelea na mapambano yao.
Nini kitafuata sasa?
Mnamo tarehe 6 Juni 2019, Sudan ilisimamishwa kutoka Umoja wa Afrika.
"Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika liliamua kwa sauti moja, kuisimamisha Sudan katika shughuli zote za AU hadi kuanzishwa kwa mamlaka ya mpito inayoongozwa kiraia, kama njia pekee ya kuinusuru nchi hiyo na migogoro yake ya sasa.”
Sudan kwa sasa iko chini ya baraza la mpito linaloongozwa na Jenerali Al Burhan tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Omar el Bashir mwaka 2019.
Serikali ya mpito ilitangaza 2024 kama mwaka wa kufanya uchaguzi mkuu.
"IGAD imekuwa ikiiunga mkono Sudan mara kwa mara, ikitetea kuondolewa kwa vikwazo na kuwezesha juhudi za amani. Hata wakati wa kusimamishwa kwa Sudan kutoka AU, IGAD ilidumisha uanachama wa Sudan.” Sheekh anaiambia TRT Afrika.
Licha ya kusitisha uanachama wake kwa muda, mgogoro wa Sudan bado unabakia kuwa suala la dharura kwa AU, ikisisitiza kuwa IGAD inapaswa kuongoza juhudi za amani nchini humo.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amewateua Waafrika watatu kuwa sehemu ya kamati ya kuangalia maswala kuhusu Sudan ili kuanzisha juhudi za kumaliza mzozo wa sasa wa kisiasa na kijeshi katika nchi hiyo.
"Wanachama wa kamati hii ya AU watafanya kazi na wadau wote wa Sudan: vikosi vyote vya kiraia, wapiganaji wa kijeshi na wahusika wa kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na IGAD, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, ili kuhakikisha mchakato wa kurejesha amani na utulivu nchini Sudan,” mwenyekiti wa tume ya AU Moussa Faki Mahamat amesema.
Dkt. David Matsanga, mtaalam wa mahusiano ya kimataifa, anasema "maslahi ya nje" yanaathiri mchakato wowote wa amani nchini Sudan.
"Inasikitisha kwamba uongozi wa IGAD na tume ya AU unaonekana kutokuwa na uwezo katika kushughulikia mzozo wa Sudan," anaiambia TRT Afrika, "hii inaweza kuhusishwa na wao kujifungamanisha na mirengo mbalimbali katika mzozo huo, ambayo inaweza kutumikia nchi za nje. maslahi ambayo yanadhoofisha umoja wa Afrika."
"Ni muhimu kutambua kwamba mzozo wa Sudan sio tu mgongano wa haiba kati ya Majenerali wawili. Unawakilisha vita pana zaidi vya kiitikadi na mwelekeo wa nje. Rais Museveni alibainisha ipasavyo kuwa Sudan ni ya Afrika, sio tu ya watu wawili waliohusika katika vita,” Dkt. Matsanga anaongeza.
Pamoja na Sudan kujisimamisha kwa muda IGAD ambayo kimsingi ni shirika la kikanda chini ya AU, haijulikani kama juhudi za AU zitaleta mabadiliko nchini humo.
"Naamini mwenyekiti wa sasa wa IGAD, Rais wa Djibouti, na Katibu Mtendaji, Dk. Workneh, watashiriki diplomasia ili kumshawishi mwenyekiti Al Burhan kufikiria upya, hasa kwa kuzingatia maoni yake ya zamani ya jitihada ya upatanishi wa IGAD katika mgogoro wa Sudan" Sheekh anaelezea kwa TRT Afrika.
IGAD bado haijatoa tamko rasmi kufuatia uamuzi wa Sudan.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema hatua ya Sudan kujitenga na IGAD ni kosa kwa sababu itamfanya Jenerali Al Burhan na nchi yake kutengwa na nchi zingine.
Wengine wanasema ni wakati wa majaribio kwa umoja huo wa kikanda, ambao pia umepata pigo jingine baada ya Ethiopia kukataa kuhudhuria mkutano wake wa Januari 18 nchini Uganda.
Ethiopia inazozana na Somalia kuhusu makubaliano iliyokuwa nayo na Somaliland kukodisha kilomita 20 kutoka Bahari Nyekundu.
Na zaidi ya yote, matumaini ya Wasudan zaidi ya milioni 7 ambao wamelazimishwa kuondoka nyumbani na mamilioni wengine wanaoishi katika hali ya wasiwasi, yanaendelea kufifia kutokana na serikali yao kuamua kujitenga na IGAD.