zana hizo zilipatikana katika bandari na uwanja wa ndege wa Mogadishu  Picha / Nisa 

Shirika la Usalama wa Taifa na Ujasusi la Somalia (Nisa) limesema limekamata shehena mbili za zana za kijeshi ambazo zinaonekana zikielekezwa kwa kundi la wanamgambo wa Al-Shabab.

Lilisema zana hizo zilipatikana katika bandari na uwanja wa ndege wa Mogadishu siku ya Alhamisi na zilihusishwa na "wafanyabiashara ambao walikuwa wameidhinishwa na serikali kuagiza bidhaa muhimu".

Katika bandari, shehena hiyo ilikuwa imefichwa katika bidhaa za kibiashara zinazoingizwa nchini, shirika hilo lilisema. Magari manne yaliyotayarishwa kusafirisha vifaa hivyo hadi kwenye kundi la wanamgambo pia yalikamatwa.

Uchunguzi kuhusiana na shehena hizo ulipelekea kukamatwa kwa watu 10 wanaohusishwa na mtandao wa magendo ya silaha unaofanya kazi ndani na nje ya nchi, taarifa ya Nisa ilisema.

" Wakala wetu wamekuwa wakifuatilia shughuli za watu hawa nchini Somalia na nje ya Somalia. Ni kufuatia ushiriki wao katika mtandao huu wa magendo. Kwa bahati nzuri, wote wako kizuizini, na hakuna aliyetoroka," Waziri wa Ulinzi Mohamed Ali Haga alinukuliwa na mashirika ya habari.

Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu maudhui ya shehena zilizokamatwa, asili yao au utambulisho wa waliohusika.

TRT Afrika