Watu kadhaa wameuawa katika mpaka wa Kenya na Ethiopia baada ya kushambuliwa na watu wenye silaha wanaoaminiwa kutoka jamii ya Dassanech kutoka Ethiopia.
Shambulio hilo linaaminiwa kuwa la kulipiza kisasi baada ya madai ya awali kuwa wavuvi kutoka upande wa Kenya katika mpaka wa Todonyang waliwavamia na kuwaua watu upande wa Ethiopia.
Hali ya taharuki imetanda katika eneo hilo huku serikali ikisema kuwa imetuma maafisa zaidi wa usalama kuimarisha amani huku ikiwaomba wakaazi kufanya subira wakisubiri maamuzi ya serikali.
Waziri wa Usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema kuwa wanashirikiana na serikali ya Ethiopia kuchunguza na kutafutia suluhu tatizo hilo.
''Serikali imeweka ulinzi wa ziada kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia kufuatia kisa kilichohusisha raia wa Kenya na jamii ya Dassanech wa Ethiopia katika eneo la Lopeimukat,'' alisema waziri Murkkomen.
Kamishna wa Kaunti ya Turkana Julius Kavita alithibitisha kutokea kwa shambulizi hilo lakini hakuweza kubaini idadi ya vifo.
"Ndio, kulikuwa na shambulio. Tumeambiwa baadhi ya watu wamepoteza maisha, na tunaharakisha kubaini ukweli kabla ya kuuweka hadharani,” Kavita alisema.
Kwa sasa Waziri Murkomen amesema kuwa serikali inatafuta ushirikiano na serikali ya Ethiopia.
''Pia tunashirikisha Serikali ya Ethiopia katika jitihada za kuleta amani kati ya jamii hizo mbili,'' aliongeza Waziri Mzurkomen.
Maafisa wa usalama wa baharini wa Kenya waliotumwa kushika doria katika Ziwa Turkana walisema giza lilitatiza operesheni ya kuwafuata wavamizi na kurejesha boti na zana za uvuvi zilizoibwa.
Todonyang ni mojawapo ya maeneo yenye rutuba ya uvuvi kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili, lakini bado ni uwanja wa vita kwa wavuvi wa Kenya na Ethiopia.