Vatican imesema kuwa kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 anaugua nimonia na maradhi mengine ya mapafu/ picha: wengine 

Vatican imesema kuwa kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 anaugua nimonia na maradhi mengine ya mapafu.

Papa Francis ni raia wa Argentina na ndiye kiongozi wa kwanza kutokea nchi zinazoendelea, kama Afrika, Asia na Marekani ya Kusini.

Barani Afrika ametambuliwa kama papa wa ujumbe wa amani hasa kwa kutembelea nchi mbalimbali akiwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki.

Novemba 2015 Papa Francis alizuru Kenya. Nchi hiyo ilikuwa imekumbwa na mashambulizi ya kigaidi 2013 na 2014 ambapo watu kadhaa waliuawa.

Katika ziara yake alitembelea eneo la vitongoji duni la Kangemi jijini Nairobi ambapo alizungumzia kuhusu kuwepo kwa ukoloni mambo leo.

Kutoka kenya alielekea Uganda kwa ziara ya siku tatu. Kando na ibada kuu alikutana na vijana , akatembelea shirika la kutoa misaada na kukutana na viongozi wa kidini nchini humo.

Novemba 2015, wakati ambapo vita vya ndani katika jamhuri ya Afrika ya kati vilikuwa vimepamba moto, papa Francis alitembelea nchi hiyo .

Kwa sehemu kubwa mzozo nchini humo ulihusisha mvutano wa kidini na ulianza 2013 baada ya rais wa nchi hiyo François Bozizé kuondolewa na waasi kupitia mapinduzi.

Maelfu waliuawa na zaidi ya watu milioni moja kuripotiwa kulazimika kuyahama makazi yao. Ujumbe wake ulikuwa kuhimiza umoja wa watu licha ya kuwa na dini tofauti.

Mwaka wa 2017 alizuru Misri ambapo alihimiza umoja huku mzozo wa kidini ukiathiri amani nchini humo .

Machi 2019 akaenda Morocco kuhimiza Amani baada ya mgogoro wa kidini pia. Ujumbe wake wa Amani ulimfikisha Sudan Kusini Februari 2023. Nchi hiyo ilikumbwa na vita kuanzia 2013 miaka miwili tu baada ya kuwa taifa huru.

Mwaka 2019 Papa Francis aliwakaribisha viongozi wa Sudan Kusini waliokuwa wakizozana, Rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar, akawabusu miguu na kuwasihi kuacha vita.

Vatican pia ilichangia kwa kuwa mwenyeji wa mazungumzao ya amani.

TRT Afrika