Mswaki wa jiti umetumiwa na vizazi vingi katika karne nyingi dunia nzima. Picha : TRT Afrika

Hassan, ameegemea ukuta wa Masjid Nur, msikiti ulioko mtaani kwake mjini Mombasa. Tayari adhan inasikika, kuwaita watu kwa sala ya alasiri . Anatafuna kijiti mdomoni.

‘’Mimi natumia mswaki huu mara tatu au nne kwa siku. Unasafisha mdomo wangu. Nimeutumia kwa miaka mingi. Tangu utotoni.’’ Anaelezea TRT Afrika.

Kijiti hicho kinaitwa Siwaak. Ni maarufu sana katika mji wa pwani ya Kenya. Mombasa. Wenyeji wanauita mswaki, kwa Kiswahili.

Mmoja baada ya mwingine utawaona wanaume wakiingia msikitini, wengi wao wanatafuna mswaki huo.

Kuna aina mbali mbali za mswaki wa jiti. Baadhi zipo kama vijiti, baadhi ni matawi na nyingine mizizi.

siwaak

Hassan anaamini, mswaki anaoutumia yeye una faida za kimatibabu.

‘Huu mswaki unaitwa Msija. Unasaidia kumaliza harufu mdomoni na kuzuia maambukizi.’ Aliongeza.

Kwingineko katika kijiji cha Korogwe, Mkoa wa Tanga, Tanzania, kilomita 260 kutoka Mombasa, Paulo Matini anaelekea kazini, kama mlinzi wa usiku.

Amevaa shuka lake la kimaasai na mdomoni anatafuna mswaki wa jiti.

‘Tangu utotoni tumekuwa tukitumia mswaki huu. Bila dawa ya meno yoyote,’ anasema.

Rahisi kuupata, rahisi kuutumia

Mswaki huu huchunwa kutoka mimea mbali mbali, kutegemea unaishi sehemu gani. Unamea nchi nyingi duniani na hutofautiana kwa rangi, ladha na maumbile yake.

Nchini India, siwaak, au mswaki hukatwa zaidi kutoka kwa mti wa Muarobaini (Azadirachtaindica); Upande wa Afrika Magharibi wanakata pia kutoka kwa mdimu (Citrus aurantafolia) na mchungwa (Citrus sinensis);

Katika maeneo mengine ya Afrika, mmea aina ya senna (Cassia vennea) ndilo chaguo maarufu. Eneo la Arabia na Afrika MAshariki, siwaak inatoka kwa mti wa Arak arak, mmea unaomea asilia katika misitu na vichaka.

Mswaki wa jiti unaweza kuwa vijiti au mizizi na inakuja na ladha, rangi au harufu tofauti Picha : TRT Afrika

Mswaki hutayarishwa kwa kukata kipande cha sentimita 15, na upana wa sentimita moja ili kurahisisha utafunaji wake.

Mle katikati kuna sehemu laini kama sponji. Baada ya kuloweka katika maji kwa dakika mbili au tatu , kijiti kinalainika na kuwezesha kutafuna kwa wepesi na unatafuna hadi uchanike chanike upande mmoja na unakuwa tayari kutumia.

Asili ya dini na utamaduni

Shirika la afya duniani WHO, lilipendekeza utumiaji wa mswaki wa jiti mwaka wa 1986, lakini baadaye 2000, kauli ya pamoja ya kimataifa juu ya afya ya mdomo ilisema kuwa kunahitajika utafiti zaidi ili kuchapisha jarida kamili juu ya athari za kusugua meno kwa mswaki wa jiti.

Hata hivyo watu wengi kutoka maeneo ya Afrika kaskazini, Mashariki na Arabia, wanahusisha utumiaji wa mswaki huu kwa ushauri wa dini ya kiislamu.

Sheikh Shaaban kutoka Nairobi anasema, ‘’Mswaki wa jiti umependekezwa kutumiwa kabla ya kusali, unapoamka asubuhi, kabla ya kuingia msikitini au kuanza safari.’’

Lakini kwa Waafrika wengi, utumiaji wakeni kutokana na utamaduni, uliopitishwa kwa vizazi.

‘Tunafundishwa na wazazi wetu na babu, tangu tukiwa wadogo sana. Nasi pia tunawafundisha watoto wetu.’’ Anasema Paulo.

Mswaki umetumiwa kwa ajili ya mafundisho ya dini ya kiislamu lakini waafrika wengi wanatumia kwa ajili ya kupokezwa kitamaduni  Picha : TRT Afrika

Utafiti mbali mbali zimefanyiwa kuhusu mswaki huo na kuna maoni ya kutofautiana juu ya faida zake.

Daktari Ramadhan Shaali, mhadhiri katika kitengo cha afya ya meno, chuo kikuu cha Zanzibar anasema kuwa japo watafiti wanatofautiana juu ya faida ya jumla ya mswaki wa jiti, baadhi ya miswaki hiyo imeonesha kuwa na kemikali zilizo na faida, japo katika viwango vidogo sana haiwezi kuwa na manufaa makubwa.

‘‘Miongoni mwa vitu muhimu vinavyo patikana katika dawa ya meno ni Floride, inayosaidia kuzuia meno kutoboka na kukinga utando wa juu wa jino, na ukitumia mswaki wa jiti pekee unajinyima fursa ya kuwa na kinga hii,’’ anasema Dkt. Ramadhan.

Madaktari hawawezi kutoa mwongozo wa hakika kwani bado utafiti zaidi unahitajika. Lakini daktari Ramadhan anasema kuwa kuna baadhi ya mambo ya kawaida yanayoweza kukudhuru katika kutumia vibaya mswaki wa jiti kama vile kujiumiza fizi na kukwaruza utando wa juu wa meno kwa kutumia nguvu nyingi wakati wa kusugua.

‘‘Unaweza kutumia mswaki wa jiti mara moja, kisha uchanganye baadaye na mswaki wa kawaida na dawa ya meno ili kupata faida kamili,’ ameongeza Dkt Ramadhan. ‘Tatizo liko pale unatumia mswaki wa jiti pekee na kutupa ule mwingine.’’

Sio lazima usafi uwe wa gharama

Katika baadhi ya maeneo, hasa ambako mimea ya miswaki inakua, au kukuzwa, utumiaji wake unakua na nafuu katika gharama, ikilinganishwa na miswaki ya dukani.

Wengi wanatumia mswaki na kuutupa kisha wanachukua mwingine baadaye, mswaki unapatikana kwa urahisi bila gharama kubwa Picha : TRT Afrika

Mfano nchini Uganda , kuna mimea aina mbili maarufu sana, kwa lugha ya wenyeji ya Luganda, wanaita Akakwansokwanso au kisayansi unajulikana kwa jina , Rhus vulgaris.

Mlinzi wa usiku Paulo, anasema, ‘ uzuri wa mswaki huu ni kuwa naweza kuutumia kisha nikautupa na baadaye nikachuna mwingine kutumia baadaye.’

Kijijini Korogwe, nchini Tanzania, mwandishi wa habari Majuka, anaketi nje ya nyumba yake wakati wa jioni. Anasema kuwa hawezi kwenda kokote bila mswaki wake wa jiti.

‘Kuna mimea mingi iliyo na ladha mbali mbali unaweza kuchagua. Unaweza kutumia mmoja asubuhi na nyingine jioni,’ anasema Majuka.

Kwa mujibu wa WHO, utumiaji wa mswaki pamoja na dawa ya meno ni pendekezo bora zaidi katika kusafisha meno.

Mswaki wa kijiti pia unaweza kufanya kazi vyema ya kupamabana na meno kutoboka, magonjwa ya mafizi au kuoza kwa jino.

Pamoja na kuwa na baadhi ya kemikali kama vile Sodium, Bicarbonate na Potasiam, unaweza kusaidia kuweka kinga katika utando wa meno na kukupa afya nzuri ya mdomo wako.

TRT Afrika