Sakata la kesi ya mauaji ya msanii wa Afrika Kusini Kiernan Forbes, maarufu "AKA" limechukua sura mpya baada ya washukiwa wawili katika kesi hiyo kupata kibali cha kuhamishwa.
Msanii huyo maarufu barani Afrika, pamoja na mwenzake Tebello “Tibz” Motsoane, waliuwawa kwa kupigwa risasi Februari 10, 2023 nje ya mgahawa mmoja nchini Afrika Kusini.
Mauaji ya msanii AKA yalitikisa tasnia ya muziki nchini Afrika Kusini na barani Afrika kwa ujumla.
Watuhumiwa watano katika kesi hiyo walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Durban mwezi Februari mwaka 2024, ikiwa ni mwaka mmoja toka yatokee mauaji hayo, huku kukiwa na madai kuwa kuna mpango wa kuwahamisha washukiwa wengine wawili waliokamatwa katika eneo la Eswatini.
Upande wa mashitaka, ukiongozwa na Wakili Lawrence Gcaba, uliwaambia waandishi wa habari kuhusu mpango wa kuwahamisha, Siyabonga na Malusi Ndimande, kutoka Eswatini haraka iwezekanavyo.
Katika hoja yao, mawakili hao walisisitiza kuwa msingi wa kesi hiyo utazidi kuimarika watuhumiwa wakiwa rumande. Mpango huo pia unahusisha uchunguzi wa simu, muamala ya kifedha na ushahidi kutoka kwa mashahidi.
Hata hivyo, siku ya Ijumaa, Mahakama Kuu ya Eswatini iliamuru kusafirishwa kwa Siyabonga na Malusi Ndimande.
Kulingana na mahakama hiyo, ndugu hao wawili waliwasilisha rufaa zao mwezi Agosti mwaka huu, ambapo ni ndani ya siku 15 kama sheria inavyosema.
Ucheleweshwaji wa kusikiliza rufani hiyo umepelekea kuhairishwa kwa kesi hiyo ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Durban.
Hakimu Mkazi huyo amesisitiza nia ya kuchukua hatua za haraka ili jalada la kesi hiyo lifungwe.
“Siwezi kuendelea kuvumilia uhairishwaji mwingine tena,” alisema Hakimu Mkazi Vincent Hlatshwayo siku ya Ijumaa.
Huku hayo yakiendelea, baba mzazi wa AKA, Tony Forbes, aliwahi kusema mwezi wa Februari kuwa haamini kama waliomuua mwanaye wapo kwenye mikono ya sheria, limeripoti Shirika la Habari la Afrika Kusini (SABC) limeripoti.
Kulingana na Forbes, familia yake bado inasaka majibu kuhusu kifo cha mpendwa wao.
Mahakama hiyo imepanga Februari 7, 2025 kama siku nyingine ya kusikiliza kesi hiyo.
Katika hatua nyingine, Hakimu Mkazi Hlatshwayo, alitupilia mbali maombi ya waendesha mashitaka wa serikali kuhusu kuhairisha kesi hiyo zaidi ya Februari 7.
“Watuhumiwa wawepo wasiwepo, lazima kesi iendelee,” alisema Hlatshwayo siku ya Ijumaa.