Watoto nchini Sudan wanazidi kuathiriwa moja kwa moja na vita vilivyoanza Aprili 2023 nchini humo/ Picha: Wengine 

Dunia inaadhimisha siku ya watoto Novemba 20, huku Sudan hali ikizidi kuwa ngumu kwa watoto kutokana na vita vita vinavyoendelea kati ya jeshi la serikali na kikundi cha Rapid support Forces.

Shirika la Matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) linalohudumu katika maeneno ya vita nchini humo linasema kuwa watoto zaidi wanaletwa wakiwa na majeraha.

"Takriban mgonjwa mmoja kati ya sita waliojeruhiwa vitani wanaotibiwa katika Hospitali ya Kufundisha ya Bashair kusini mwa Khartoum tangu Januari 2024 wamekuwa chini ya umri wa miaka 15," MSF imesema.

"Wengi walijeruhiwa kwa risasi, milipuko na majeraha ya risasi. Madaktari pia wana wasiwasi kuhusu ongezeko la watoto wanaofika hospitalini wakiwa na utapiamlo," Shirika hilo limesema.

Licha ya vita Wizara ya Afya na Shirika la Kutetea Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF zimeshirikiana kuwapa watoto chanjo dhidi ya malaria/ Picha UNICEF Sudan

Kikosi cha MSF kinachofanya kazi pamoja na wafanyakazi wa hospitali kimewatibu zaidi ya wagonjwa 4,214 kutokana na majeraha na kiwewe kilichosababishwa na ghasia, ikiwa ni pamoja na milio ya risasi na milipuko ya mabomu. Kati ya hawa, 16% walikuwa watoto chini ya miaka 15.

Mifano ya watoto walioathiriwa

Mnamo 2024 MSF inasema timu zake za dharura zilitibu watoto 314 waliolazwa katika Hospitali ya Mafunzo ya Bashair, Khartoum, kutokana na majeraha ya milipuko ya bomu.

Hii ni mojawapo ya hospitali ambazo bado zina uwezo wa kutoa huduma kusini mwa Khartoum, inatoa huduma za dharura na upasuaji pamoja na huduma za afya ya uzazi.

Baadhi ya watoto 3,500 wanaosaidiwa kupata elimu katika jimbo la Kassala ambalo kidogo lina usalama./ Picha: UNICEF 

"Mtoto kwa jina Riyad wa miezi 18 aliletwa kwenye chumba cha dharura baada ya risasi kumpiga upande wake wa kulia alipokuwa amelala nyumbani kwa familia yake," alisema Dkt Moeen, kiongozi wa timu ya matibabu ya MSF.

MSF imebadilisha jina la daktari kwa ajili ya usalama wake.

Riyad ni mmoja wa watoto 314 waliotibiwa kutoka na majeraha ya risasi na milipuko mnamo 2024.

"Timu ya matibabu ilipambana kwa saa nne kumtuliza. Kutokana na upotevu mkubwa wa damu, uwezekano wa yeye kunusurika upasuaji ulikuwa hamsini na hamsini.”

Timu hiyo iliweza kuzuia kuvuja damu, hata hivyo risasi ilibaki kifuani mwake. Madaktari wanasema haijulikani itachukua muda gani kabla ya jambo lolote kufanywa kuhusu hili.

Hospitali haina uwezo wa juu wa upasuaji, kutokana na sababu ya kizuizi cha utaratibu katika kutuma vifaa vya upasuaji tangu Oktoba 2023.

Madakitari hao wanasema mwishoni mwa Oktoba zaidi ya wagonjwa 30 waliojeruhiwa katika vita walikimbizwa katika Hospitali ya Bashair kwa siku moja kufuatia mlipuko katika soko lililo umbali wa chini ya kilomita moja.

Kumi na wawili kati ya walioletwa kwenye chumba cha dharura walikuwa watoto chini ya miaka 15.

Wanasema wengi walikuwa wameungua.

Msichana mmoja wa miezi 20 aliingia akiwa na vipande vya makombora kichwani mwake.

Wanasema wakati alipolazwa kwa uangalifu kwenye meza ya X-ray, sehemu ya fuvu dhaifu la kichwa kidogo ilianguka.

"Kesi kama hizi ni za kawaida," anasema Dkt Moeen.

“Nashukuru msichana huyo mdogo aliokoka. Wengine hawana bahati sana.”

MSF inasema kuwaelekeza wagonjwa nje ya eneo hilo pia ni vigumu sana kwani njia za usafiri zimeharibiwa au ni hatari sana.

TRT Afrika