Shirika la Wakimbizi Duniani UNHCR linakadiria kuwa, zaidi ya watu milioni 117 wamelazimika kuyahama makazi yao duniani kote./ Picha : Reuters 

Na Dayo Yussuf

‘’Ilikuwa mwendo wa saa kumi alasiri. Watu wenye silaha walitokea ghafla na kutupiga na wengine wakauawa.’’

Kumbukumbu ya kutisha iliyochapishwa katika mawazo ya Najwa milele. Hiyo ndiyo siku ambayo yeye na familia yake walitupwa katika maisha ya wakimbizi.

Najwa, 30, alilazimika kutoroka na watoto wake watatu wakati mapigano kati ya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Rapid Support Forces (RSF) yakipamba moto karibu na kambi ya Al-Hasahisa, Zalingei, Sudan, mwishoni mwa mwaka wa 2023.

Sasa anaishi katika gofu la benki iliyotelekezwa na kuporwa mjini pamoja na watu wengine thelathini waliokimbia makazi yao.

"Tunaishi katika mazingira haya bila paa, na hatuna chakula," anaiambia TRT Afrika. "Lakini hatujawahi kupokea msaada wowote, hata kipande cha sabuni. Mvua zikinyesha, hatujui pa kwenda." Anaeleza.

Tangu Aprili 15 2023, wakati mapigano makali yalipozuka kati ya vikosi hivyo viwili, Sudan imeripoti mojawapo ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu ambapo zaidi ya watu milioni 8.6 wamelazimika kuyahama makazi yao, wakiwemo wakimbizi wa ndani (IDPs), wanaotafuta hifadhi na wakimbizi.

Hii ilizidisha hali mbaya zaidi ambayo tayari ilikuwa ya kutamausha iliyosababishwa na migogoro ya kikabila iliyokuwepo pamoja na ukame ambao wengine wengi walikuwa wamekimbia hapo awali.

Shirika la MSF au Madaktari wasio na Mipaka ambalo linafanya kazi kwa karibu na familia kama Najwa's nchini Sudan linakadiria kuwa karibu milioni 6.5 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi.

Takwimu zinatisha lakini cha kusikitisha ni kwamba hii ni sehemu ndogo tu ya picha ya ulimwengu.

Shirika la Wakimbizi Duniani UNHCR linakadiria kuwa, zaidi ya watu milioni 117 wamelazimika kuyahama makazi yao duniani kote.

mbali na Sudan, 2023 na 2024 ilishuhudia moja ya migogoro mbaya zaidi ya wakimbizi kutokana na mapigano Mashariki mwa DRC, Myanmar, Ukrain na Palestina./ Picha : Reuters 

Usalama kwa mashirika ya misaada

Miongoni mwao ni karibu wakimbizi milioni 43.4, karibu asilimia 40 ambao wako chini ya umri wa miaka 18.

Licha ya Sudan kuwa mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya watu kuhama makwao duniani, mashirika hayajarejea nchini humo tangu kuondoka wakati vita vilipoanza.

Wengi wao walilazimika kuondoka kutokana na mashambulizi yaliyowalenga na uporaji kutoka kwa makundi yanayopigana ambayo katika baadhi ya matukio yaliishia katika mauaji ya wafanyakazi wa mashirika hayo ya kibinadamu.

‘’Moja ya changamoto kubwa ni hali ya usalama,’’ anasema Igor Garcia, Mshauri wa Mawasiliano wa MSF. ‘’ Mashambulizi ya anga, makombora na ufyatulianaji wa risasi yanafanyika kila siku katika maeneo tofauti yaliyoathiriwa na mzozo huo. Watu wanalazimika kukimbia, mara nyingi mara kwa mara. Na mara tu wanapofika mahali salama, kuna usaidizi mdogo sana wa kibinadamu unaopatikana,’’ anaiambia TRT Afrika.

Kwa zaidi ya miezi sita, Aissa na familia yake, ambao pia ni wakimbizi katika kambi ya Al-Hasahisa huko Zalingei, Jimbo la Darfur ya Kati, Sudan wameishi katika kontena moja katika kituo cha zimamoto cha Zalingei.

Nyumba zao pia zilishambuliwa na vikundi vya wapiganaji mnamo 2003.

‘’Tulifukuzwa na kulazimishwa kuondoka,” Aissa, 50, aliiambia TRT Afrika. “Baadhi ya wanaume wetu waliuawa. Wengine wamewekwa kizuizini. Vitu vyetu vilichukuliwa na kuibiwa. Tulipokuwa tukiondoka, tulizuiwa na watu wenye silaha na tukalazimika kungoja hadi asubuhi. Walifunga watu na kuwapiga wavulana wachanga.” Anasema.

mwaka huu, Siku ya Wakimbizi Duniani inaangazia mshikamano na wakimbizi - kwa ulimwengu ambapo wakimbizi wanakaribishwa./ Picha : MSF Sudan

Kadiri idadi, muda na ukubwa wa migogoro inavyoongezeka, ndivyo idadi ya watu wanaolazimika kukimbia kila mwaka inavyoongezeka.

UNHCR inasema mbali na Sudan, 2023 na 2024 ilishuhudia moja ya migogoro mbaya zaidi ya wakimbizi kutokana na mapigano Mashariki mwa DRC, Myanmar, Ukrain na Palestina.

Kwa bahati mbaya, licha ya hali ya kukata tamaa, mwelekeo wa kimataifa umeonyesha kuna ongezeko la chuki dhidi ya wakimbizi hasa kutoka nchi zinazowahifadhi.

Mamia ya visa kama si zaidi vinaripotiwa kila siku vya mashambulizi dhidi ya wakimbizi na kutoridhika kwa jumla miongoni mwa mataifa yanayowahifadhi na kusababisha mashambulizi dhidi ya wakimbizi na katika baadhi ya visa kukatwa ufadhili wa programu za wakimbizi.

‘’Nchini Sudan, pande zote mbili zinazopigana zinafanya kuwa vigumu sana kufanya kazi ili kutoa msaada unaohitajika sana. Kwa upande mmoja, katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na RSF mara nyingi kuna hali ya ukosefu wa usalama na wafanyakazi wa afya hupokea shinikizo nyingi. Kwa upande mwingine, Serikali ya Sudan kwa makusudi inawanyima vibali vya usafiri wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kufikia baadhi ya maeneo, hasa katika mstari wa mbele,’’ anasema Garcia wa MSF.

Mshikamano na Wakimbizi

UNHCR inasema, mwaka huu, Siku ya Wakimbizi Duniani inaangazia mshikamano na wakimbizi - kwa ulimwengu ambapo wakimbizi wanakaribishwa.

‘’ Mshikamano unamaanisha kuweka milango wazi, kusherehekea nguvu na mafanikio yao, na kutafakari changamoto zinazowakabili,’’ inasema taarifa ya UNHCR.

UNHCR inasema kunawakimbizi milioni 43.4, ambapo karibu asilimia 40 kati yao wako chini ya umri wa miaka 18/ Picha : MSF Sudan

Ajenda hii inakaribishwa na watu kama Aissa walioko kambini Sudan.

Anasema, kutokana na kukatika kwa misaada ya kibinadamu, yeye na familia yake wanatatizika kupata hata mlo mmoja kwa siku.

Wakiishi kwa kufanya kazi zisizo za kawaida hapa na pale, bado hawana ufikiaji ufaao wa maji, chakula au huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na matibabu.

"Hakuna njia ya kupata pesa," anaiambia TRT Afrika. "Tunatoka tu na kuzurura mjini. Tukipata mtu unayeweza kumfulia nguo, unaifua angalau upate pesa,” anasema.

MSF sasa inatoa wito kwa pande zinazopigana kuhakikisha ulinzi wa raia, wafanyakazi wa afya na vituo ili kuwaruhusu kupata njia ya kupitisha misaada ya kibinadamu isiyozuiliwa ili kufikisha misaada muhimu ya kwa wale wanaoihitaji zaidi.

Na wakati dunia inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani, kuna hofu miongoni mwa wafanyakazi wa kibinadamu kwamba mwangaza mkubwa zaidi ya kimataifa utawekwa kwa Palestina na Ukrain, na kusahaulika mgogoro mkubwa unaoendelea Sudan na DRC.

‘’Ni watu wachache sana wanaozungumza kuhusu kinachoendelea Sudan. Sudan na watu wa Sudan wanastahili kuzingatiwa zaidi, na ni wajibu wetu kuzungumza kuhusu kile kinachotokea Sudan na kuchukua hatua,’’ anasema Garcia wa MSF.

TRT Afrika