Coletta Wanjohi
TRT Afrika Istanbul, Uturuki
Katika pembe ya Afrika, mzozo nchini Sudan umewalazimu Fatma Ibrahim na binti zake mapacha kutafuta hifadhi katika kambi ya Kalma ya Darfur Kusini, ndani ya nchi hiyo.
Hapa mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao hawajui ni lini watarudi makwao.
Mapigano kati ya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka yaliyoanza Aprili 2023 yameleta hali ya kukata tamaa kwake na kwa wanawake wengine kwenye kambi hizo.
Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa zaidi ya watu milioni 8 wamehamishwa kutoka katika makazi yao. Wakati zaidi ya milioni 2 wamekimbilia nchi jirani, huku wengine zaidi ya milioni 6.2 kama Fatma wamesailia kuwa wakimbizi wa ndani.
"Baada ya kujifungua mapacha wangu mnamo Disemba 2023, sikuweza kuwanyonyesha kwa sababu nilikosa chakula cha kutosha," anaeleza.
Wasichana wake walikabiliwa na utapiamlo na ilibidi walazwe katika kituo cha afya huko Kalma, Darfur Kusini.
Kama ilivyo katika sehemu nyengine za dunia migogoro barani Afrika ina athari kubwa kwa wanawake na watoto.
Katika mkutano wake wa Disemba 2023 kuhusu Wanawake na Amani na Usalama barani Afrika, Umoja wa Afrika ulionyesha wasiwasi juu ya hali ya migogoro inayoendelea katika bara hilo, zikiwemo Burkina Faso, Chad, DRC, Niger, Mali, na Sudan.
Umoja wa Afrika ulitoa wito kwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika mchakato wa amani nchini Sudan.
Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye hili halijawezekana kwa sababu juhudi za mazungumzo kwa ajili ya Sudan zimekwama.
Fatma anasema hajui hata jinsi ya kuwa sehemu ya mchakato wa amani kwa nchi yake, na anachotaka ni kurejea nyumbani.
Wanawake ni wachache kwenye meza ya amani
Katika nchi ambazo migogoro imepungua na sasa zinajitahidi kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa, kama vile Ethiopia na Sudan Kusini, wanawake na wasichana wengi bado hawajapona kutokana na makovu ya kuhama makazi yao, unyanyasaji wa kijinsia pamoja na hofu ya maisha yao.
Umoja wa Afrika una wasiwasi kuwa wanawake wanasalia kuwa na uwakilishi mdogo kama wapatanishi, wajumbe, watia saini na waangalizi wa mchakato wa amani barani Afrika.
"Leo tunasema kwamba bila wanawake kwenye meza hakuna meza ya amani kwa hivyo tunachohitaji kufanya ni kubadili meza," Bineta Diop, mjumbe maalum wa AU wa Wanawake kwa amani na usalama, anaiambia TRT Afrika.
Mwaka 2014 Umoja wa Afrika ulimteua Bineta Diop kupaza sauti za wanawake katika kuzuia, kudhibiti na kutatua migogoro, pamoja na kutetea ulinzi wa haki zao, na kukomesha unyanyasaji wa kijinsia barani.
“Kwa nini tunawekeza kwa wale wanaoshika bunduki? Tunashindwa kwa sababu tunawekeza katika upande usiofaa, kwa hivyo tunahitaji mabadiliko ya dhana na kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya mchakato wa kutatua matatizo,” Diop anaongeza.
Anita Kiki Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini anasema ni muhimu kwa mashirika ya kimataifa kusikiliza na kufuata mawazo ya wanawake walioathiriwa na migogoro.
Anakumbuka alipokwenda kutembelea vikundi vya wanawake katika mkoa wa Darfur nchini Sudan siku za nyuma, hali hiyo ilimfundisha kuwa wanawake daima wanajua jinsi mvutano katika jumuiya yao unavyoweza kumaliza.
“…Mama mmoja ambaye alikuwa kiongozi wa vikundi vya wanawake alinitazama tu na kusema ‘ukitaka kutusaidia fanya jambo moja, kuna baadhi ya wanaume wameshika bunduki kwenye kona ya barabara kuu, waondoe na tunaweza kuendelea na biashara yetu, hatuhitaji kitu chengine chochote…” Kiki alieleza katika mjadala wa mtandaoni kuhusu wanawake katika amani na usalama.
"Kwa hivyo unaweza kwenda kwa wanawake waliaothiriwa na vita ukifikiria kuwa unatoa pesa nyingi na labda wanachotaka ni rahisi sana na haigharimu chochote," alisema.
Angalau nchi 30 za Kiafrika - zaidi ya nusu ya nchi katika bara hilo zimepitisha mipango ya Kitaifa ya kujumuisha ajenda ya Wanawake katika Amani na Usalama. walakini, utekelezaji kamili bado unahitajika.
"Tunachozungumza ni jinsi gani tunafanya kazi kwa vitendo na uwajibikaji?" Diop anauliza.
Umoja wa Mataifa unasema ushiriki wa wanawake barani Afrika katika michakato ya amani na siasa mara nyingi hupingwa na kanuni za kitamaduni.
"Kuna ukosefu wa uratibu na ushirikiano wa watendaji mbalimbali wanaoshughulikia Wanawake, Amani na Usalama katika ngazi ya kikanda na kitaifa. Mashirika ya kiraia ya wanawake yanayofanya kazi katika ujenzi wa amani, kuzuia mizozo, yana ufadhili duni na hayajajumuishwa vyema katika mijadala mikuu ya sera kuhusu amani na usalama katika kanda,” UN inasema.
Wataalamu wanasema kuwa Afrika lazima iwekeze kadiri inavyowezekana katika elimu ya wanawake na vijana kutoka umri mdogo na kuwapa ujuzi katika sekta tofauti. Hii wanasema itawapa uwezo wa kutoa suluhu tofauti zitakazozuia mizozo na endapo mchakato wowote wa amani katika jamii yao utahitajika.
"Wanawake wanapoongoza, tunakuwa na matokeo mazuri kwa watu. Tusiangalie tu wanawake kama waathiriwa, ndiyo ni waathiriwa wakati mwingi, lakini pia ni chanzo cha mabadiliko,” Diop anaiambia TRT Afrika.
"Ikiwa tutakosea kutowaongeza wanawake katika michakato ya amani, makubaliano yoyote yatashindwa na tuna utafiti na data inayoonyesha hilo. Kwa hivyo, tunachohitaji kufanya ni kuhakikisha kuwa wanawake wanakuwepo."
Hata hivyo, kwa wale wanawake walioathirika moja kwa moja na migogoro kama vile Fatma, hofu yao kuu ni maisha yao yatakuwaje ikiwa vita havitakomeshwa?