Nyaraka zilizowasilishwa na Wizara ya Fedha mbele ya Kamati ya Bunge ya Bajeti zimefichua kuwa msaada wa Uganda kutoka kwa wafadhili unatarajiwa kushuka kutoka dola 732,963,975 mwaka 2023/24 hadi dola 7,627,464.02 pekee katika bajeti ijayo ya 2024/25.
Waziri wa Afya, Jane Aceng alionya kuwa ufadhili wa katika sekta ya afya unatarajiwa kushuka kwa 49%.
Alikataa kuhusisha kushuka kwa ufadhili na kupitishwa kwa sheria ya kupambana na mapenzi ya jinsia moja ya Mei 2023.
"Najua katika mawazo yenu, munafikiri ni Sheria ya Kupinga mapenzi ya jinsia moja ndiyo chanzo, lakini sivyo," Waziri wa Afya, Jane Aceng aliambia kamati ya bunge.
" Ufadhili umekuwa ukishuka na nimekuwa nikiwasilisha hili kwa sababu wafadhili hawawezi kutuunga mkono milele. Kweli, hivi majuzi, tulisikitishwa pale PEPFAR ilipotangaza kujitoa, kukawa na mjadala mzito kwenye baraza lao la mawaziri, "
Bunge la Uganda lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Kupinga mapenzi ya jinsia moja Mei 2023 na serikali ya Marekani ikatishia kuondoa ufadhili kwa Uganda kupitia Mpango wa Rais wa kupambana na Ukimwa maarifu kama PEPFAR.
Marekani imesema haitatimiza tishio lake, huku kukiwa na hofu kati ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, jinsi wataendelea kupata matibabu yao ambayo imekuwa ikitegemea ufadhili wa PEPFAR.
"Kwa hiyo suala hapa ni kwamba, tunatakiwa kujipanga huku wafadhili wakiendelea kupungua, na ni kweli wanapungua. Na tayari nimeshawaeleza kuwa fedha zote za afya ya umma zinatoka kwa wafadhili, hivyo ni suala nyeti sana,”Waziri Aceng aliambia kamati ya bunge.
Vikwazo kutoka Marekani
Marekani imeiondoa Uganda kwenye utaratibu wa kunufaika na mpango wa biashara wa AGOA kuanzia Januari 2024, baada ya nchi hiyo kupitisha sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja mwezi Mei mwaka uliopita.
AGOA ilizinduliwa mwaka wa 2000, na Marekani kwa nia ya kuruhusu kuingiza bidhaa za Afrika katika soko la Marekani bila kulipia ushuru. Hii ilikuwa na nia ya kuinua nchi za Afrika kiuchumi huku zaidi ya bidhaa 1800 zikiwa katika orodha hiyo.
Lakini sasa Marekani imeamua kuiondoa Uganda katika mkataba huo kuanzia Januari 2024 ikidai Uganda imekiuka haki za kibinadamu.
Uganda imekashifu Marekani ikionya hatua hiyo itawadhuru hasa wakulima ambao walikuwa wanategema kuuza bidhaa zao Marekani kupitia mfumo huo.