Serikali ya Rwanda inasema inasikitishwa na uamuzi wa Burundi wa kuamua kufunga mipaka.
"Serikali ya Rwanda imefahamu kupitia vyombo vya habari kuhusu uamuzi wa upande mmoja wa Serikali ya Burundi kufunga tena mipaka yake na Rwanda," imesema katika taarifa ya serikali ya Rwanda.
" Uamuzi huu wa bahati mbaya utazuia usafirishaji huru wa watu na bidhaa kati ya nchi hizo mbili, na unakiuka kanuni za ushirikiano wa kikanda na utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki," Rwanda imeongezea.
Hatua hii ya Burundi ya kufunga mipaka yake na nchi ya Rwanda inakuja siku chache baada ya Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kuishutumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi wa Burundi wa Red Tabara.
Tarehe 30 mwezi Disemba mwaka 2023, Rwanda ilipinga madai haya yalipojitokeza.
"Serikali ya Rwanda inakataa maoni ya Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye anayedai kuwa Rwanda inaunga mkono makundi ya waasi wenye silaha ya Burundi walioko mashariki mwa DRC," alisema Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda katika taarifa iliyotolewa wakati huo.
Hii ni baada ya waasi hao kufanya shambulio katika eneo la mpakani mwa Burundi na DRC na kuwauwa raia wasiopungua 20.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye aliishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa vuguvugu la Burundi la RED-TABARA lenye makao yake mashariki mwa DRC.
Rais Ndayishimiye ameilaumu Rwanda kwamba imeshindwa kutoa ushirikiano na kukataa kuikabidhi Burundi watu wanaotuhumiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi mwaka wa 2015 na ambao Serikali ya Burundi inadai ndio wamekuwa wanapanga mashambulizi dhidi ya Burundi wakiwa na ngome yao mjini Kigali.
Rwanda tayari ina mvutano na jirani yake mwingine Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambapo DRC imekuwa iliilaumu kwa kuunga mkono kikundi cha waasi wa M23. Tuhuma ambazo Rwanda pia imekuwa ikizikana siku zote.
Uasi wa M23 ulianzishwa mwezi Aprili 2012, ukitokea kutoka kundi la waasi la Congress for the Defence of the People, kundi la waasi ambalo lilipigana na serikali ya DRC kati ya mwaka 2006 na 2009.