Bodi ya Madini, Petroli na Gesi ya Rwanda (RMB) imetangaza kugundua visima 13 vya mafuta katika Ziwa Kivu kufuatia utafiti uliofanyika katika eneo hilo.
Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kujua wingi wa mafuta na gharama zinazohusika katika uchimbaji wake.
“Habari njema ni kwamba tuna mafuta. Utafiti wa awali katika Ziwa Kivu ulifichua kuwepo kwa visima 13 vyenye uwezo wa kutoa mafuta,” Mkurugenzi Mtendaji wa RMB, Francis Kamanzi, aliwaambia wabunge Jumatano, Januari 15, 2025.
Kamanzi alieleza hayo wakati wa majadiliano kati ya Kamati ya Bunge la Utawala, Usawa wa Jinsia na Wizara ya Mazingira.
Bodi hiyo katika taarifa imefafanua kuwa utafiti wake kati ya 2021 na 2022 ulionyesha kuwa "bonde la Ziwa Kivu - sehemu ya mfumo mpana wa bonde la ufa la Afrika Mashariki - lina unene wa kina cha karibu kilomita 3.5 ambapo kunaweza kuwa chanzo cha haidrokaboni.
Imesema Utafiti ulibainisha maeneo 13 ziwani yanayoweza kuchimbwa ili kuthibitisha kuwepo na asili ya haidrokaboni.
Juhudi za utafiti wa kutafuta mafuta nchini Rwanda zilianza miaka iliyopita lakini zilisitishwa mwaka wa 2014.
Zilianza tena baada ya kampuni ya Black Swan Energy ya Canada kugundua kuwa sehemu za Kivu Mashariki zinaweza kutoa mafuta na gesi kwa urahisi.
Uwepo wa gesi aina ya methane katika Ziwa Kivu ulikuwa kiashiria cha awali cha uwezekano mkubwa wa mafuta, kwani methane mara nyingi hupatikana pamoja na mafuta.
Kwa sasa kampuni mbili - KivuWatt na Shema Power Lake Kivu (SPLK) hufua gesi ya methane kutoka Ziwa Kivu ili kuzalisha hadi MegaWati 92 za umeme.
Wizara ya Madini ya Rwanda katika tovuti yake imewaalika wawekezaji ambao wana uwezo wa kufanya utafiti zaidi kuhusu mafuta.
Inasema, "Wawekezaji katika sekta ya nishati na gesi wanahimizwa kujitosa katika utafiti wa hali ya juu wa Bonde la Ziwa Kivu. Lengo ni kuungana na wenzetu katika kanda kama wadau katika sekta ya mafuta."
Nchi jirani ya Uganda iligundua mafuta katika eneo la Ziwa Albertine, magharibi mwa nchi.