Wavuvi wakiwa katika maboti yao wakivua samaka usiku katika Ziwa Kivu, Kibuye, magharibi mwa Rwanda. / Picha: AFP

Rwanda imesaini makubaliano ya kimataifa ya kukabiliana na uvuvi haramu na usiodhibitiwa ambao unatishia bayoanuwai na uzalishaji wa samaki katika vyanzo vya maji.

Mkataba huo unaounganisha zaidi ya nchi 70, zinazoongozwa na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO).

Makubaliano ya WTO kuhusu Ruzuku ya Uvuvi ni kilele cha zaidi ya miaka 20 ya mazungumzo.

Uidhinishaji wa Rwanda umefanyika wakati wa Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa WTO unaofanyika kuanzia Februari 26 hadi 29, 2024 katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

"Mkataba huu ni mzuri kwa sababu duniani kote, dola bilioni 24 zinatumika katika uvuvi haramu na uvuvi wa kupita kiasi ambao unatishia sana viumbe hai, vyanzo vya uvuvi, na maisha ya jumuiya za wavuvi," Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Jean-Chrysostome Ngabibitsinhe alisema huku akiwakilisha maamuzi ya Rwanda.

Zaidi ya nyavu 30,000 za uvuvi haramu na boti zipatazo 3,000 zilinaswa katika Ziwa Kivu katika kipindi cha kati ya mwaka 2020 hadi 2022, katika wilaya za Rubavu, Rutsiro, Karongi, Nyamasheke na Rusizi, gazeti la New Times limebaini.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti wa Wanyama na Teknolojia wa Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali ya Wanyama ya Rwanda (RAB) Solange Uwituze alisema kuwa nyavu haramu 13,449 zinazojulikana kama Kaningini na vyandarua 1,821, boti 1,252 na majangili 232 zilitaifishwa mwaka 2021/22.

Uzalishaji wa samaki katika Ziwa Kivu uliongezeka kidogo kutoka tani 18,756 mwaka 2020/21 hadi tani 19,479 mwaka 2021/22. Katika mwaka 2020/2021 na 2021/2022, uzalishaji wa kitaifa ulikuwa tani 41,664 na 43,650 mtawalia.

Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO , linaonyesha kuwa asilimia 35 ya samaki wanaweza kutoweka iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Zaidi ya watu milioni 12 wa Afrika wanategemea uvuvi na Afrika inapoteza dola bilioni 2.3 kila mwaka kutokana na uvuvi usiodhibitiwa huku asilimia 30 ya akiba ya samaki ikiharibiwa.

TRT Afrika