Mswada huo unaharamisha uvunaji, matumizi na uuzaji wa ‘miti ambayo haijakomaa / Picha Rwanda Development Board

Bunge la Rwanda limepitisha mswada unaosimamia misitu na miti.

Mswada huo unapendekeza masharti makali, ikiwa ni pamoja na kuzuia uvunaji wa ‘miti michanga,’ na kuwalazimu wakazi kutafuta vibali vya kuruhusiwa kukata miti iliyokomaa.

Pamoja na vifungu vyengine, mswada huo unaharamisha uvunaji, matumizi na uuzaji wa ‘miti ambayo haijakomaa,’ isipokuwa ikiwa imeidhinishwa na Wizara inayosimamia Mazingira kwa ‘sababu maalum.’

Mswada huo unatambua mti usiokomaa kama mti wenye upana chini ya sentimita 20 kipimo cha sentimita1.30 kutoka ardhini, kulingana na tafsiri.

Hata hivyo, mswada huo haukueleza nini kingetokea iwapo baadhi ya miti itashindwa kufikia upana wa shina kutokana na sababu mbalimbali kama vile aina ya udongo au upungufu wa virutubishi.

Mswada huo unasema kuwa wakazi hawatakiwi kuwa na leseni ya kuvuna misitu yenye chini ya hekta mbili chini ya sheria iliyopo, watalazimika kuwa na kibali kabla ya kustahili kuvuna mti wowote kwa mujibu wa mswada mpya.

Mswada huo unalenga kulinda zaidi mazingira na kuzuia athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kulingana na Bunge.

Itakapotangazwa, itachukua nafasi ya sheria inayosimamia usimamizi na matumizi ya misitu, ambayo ilitungwa mwaka 2013.

Mswada huo unalenga kuunga mkono juhudi za Rwanda za kutumia fursa tofauti kama vile biashara ya hewa mkaa katika misitu (fedha za kaboni), kupitia sheria, kulingana na Wizara ya Mazingira.

TRT Afrika