Serikali ya Rwanda inasema kuna haja ya kuongeza juhudi za kupunguza udumavu miongoni mwa watoto hadi asilimia 15 kutoka viwango vya sasa vya asilimia 21.7 hasa katika mkoa wa Kusini.
Juni mwaka 2023, Rwanda ilizindua mpango wa kina wa miaka miwili unaolenga kupunguza udumavu na kufikia Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko.
Kulingana na Nadine Umutoni Gatsinzi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Maendeleo ya Watoto (NCDA), lengo ni kupunguza udumavu hadi asilimia 19 ifikapo mwisho wa 2024.
Gavana wa mkoa wa Kusini nchini Rwanda Alice Kayitesi amesema tayari kuna mfano kutoka maeneo mengine nchini unaoonyesha uwezekano wa malengo hayo kufikiwa.
"Udumavu miongoni mwa watoto ulikuwa asilimia 36 katika Wilaya ya Kamonyi mwaka 2015. Hili ni somo ambalo wilaya nyingine zinaweza kuondokana na udumavu," alisema.
Utafiti wa Afya ya Idadi ya Watu wa Rwanda mwaka 2019-2020 umebaini kuwa mtoto 1 kati ya 3 walio chini ya miaka 5 amedumaa, yaani, ni kimo chake ni tofauti na uhalisia wa umri wake.
Majimbo ya Magharibi na Kaskazini yalikuwa na kiwango kikubwa zaidi cha udumavu.
Kutafuta suluhisho
Udumavu husababishwa na lishe duni ya mama, lishe duni kwa watoto, maambukizi ya mara kwa mara yanayosababisha kuharisha, ukosefu wa huduma ya matibabu, na ubongo kukosa uchochezi usiofaa ili kuhimiza ukuaji wa kawaida.
Kulingana na Utafiti wa sita wa Demografia na Afya wa Rwanda (RDHS 2020), kiwango cha kitaifa cha udumavu wa watoto kilipungua kutoka asilimia 38 mwaka 2015 hadi asilimia 33 mwaka 2020.
Serikali inalenga kupunguza kiwango hiki hadi asilimia 19 ifikapo mwisho wa 2024, na juhudi zimewekwa ili kupunguza kiwango cha udumavu hadi asilimia 15 ifikapo 2029.
Moja ya mipango ya serikali hiyo ni Mpango wa Lishe kwa Jamii, unaoshirikisha jamii katika elimu ya lishe na usaidizi wa vitendo.
"Kupitia maonyesho ya upishi, elimu ya msingi ya uzazi, na vipimo vya kawaida vya lishe, mpango unatambua watoto wenye utapiamlo mapema na kuwapeleka kwenye vituo vya afya kwa matibabu," alisema.
"Mpango huo pia unahusisha kuwafunza watu kuanzisha bustani za nyumbani, kuhakikisha kuwa kila kaya inaweza kupata mboga mboga, na hivyo kuchangia lishe bora kwa ujumla," aliongeza.
Pia kuna mpango wa kutoa maziwa kwa watoto wenye utapiamlo wanaotambuliwa kupitia wahudumu wa afya wa jamii.
Kwa mujibu wa Jacques Nsengiyumva, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Rwanda Women Adolescent and Child Health Initiative (RWACHI), kuelimisha na kusaidia kaya zilizo katika mazingira magumu ni muhimu ili kutokomeza udumavu miongoni mwa watoto.
"Vikundi vya kuweka akiba vinapaswa kuundwa na kutumika kama majukwaa ya elimu kuhusu kutokomeza udumavu na ukulima mdogo," alibainisha.