Maeneo ya starehe yataruhusiwa kufanya biashara usiku kucha Ijumaa, wikiendi na siku za mapumziko. Picha: Wengine 

Kama ilivyo katika nchi nyengine barani mwezi wa Disemba huvutia watu tofauti kwenda nchini Rwanda. Huku wengine wakirudi nyumbani kusherehekea na jamaa zao msimu wa Krismasi, kuna watalii ambao hutumia mwezi wa Disemba kutembelea maeneo ya utalii nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Rwanda imeongeza muda wa sehemu za starehe kufanya kazi wakati wa msimu wa Sikukuu mwezi huu wa Disemba.

Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) imesema hii inalenga kurahisha sherehe za msimu wa Krismasi kwa njia ambayo itadumisha heshima katika jamii.

Wakati wa msimu wa sherehe, kumbi za sherehe, mikahawa, hoteli, vilabu vya usiku, na sherehe binafsi zinaruhusiwa hadi saa nane alfajiri kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi.

Maeneo hayo yataruhusiwa kufanya biashara usiku kucha Ijumaa, wikiendi na siku za mapumziko ya umma.

Mabadiliko hayo yameanza kufanya kazi Jumanne, Disemba 10 na yataendelea hadi Januari 5, 2025.

Hata hivyo, Serikali imeomba wananchi kuheshimu kiwago cha kelele kinachoruhusiwa wakati wa usiku ili kutosumbua amani ya wananchi wengine.

"Kanuni za kupima kelele zinaendelea kutumika, na mashirika yanakumbushwa kuzingatia wajibu wao, ikiwa ni pamoja na kutowapa watoto vinywaji visivyowafaa,” RDB ilisema katika taarifa yake.

Mnamo Agosti 2023, RDB ilianzisha kanuni zilizosasishwa zinazosimamia shughuli za biashara ya usiku, ikiwa ni pamoja na maeneo ya burudani.

Mwongozo huo, unaotokana na azimio la Baraza la Mawaziri la tarehe 1 Agosti 2023, kuanzia Septemba 1, 2023, kufungwa kwa huduma zote zisizo za lazima kuanzia saa saba za usiki kwa siku za kazi na saa nane za alfajiri wakati wa wikiendi yaani Ijumaa na Jumamosi.

TRT Afrika