Serikali ya Rwanda inapendekeza kupunguza umri wa watu kuoa na kuolewa kutoka miaka 21 hadi 18.
Sheria hii iwapo itapita basi raia wa Rwanda ambaye atakuwa ametimiza umri wa miaka 18 ataweza kuruhusiwa kuoa kisheria, iwapo atawasilisha ombi kwa mamlaka husika na kutoa sababu halali.
Bunge inajadili pendekezo hili.
Hii ni mojawapo ya mabadiliko mapya yaliyopendekezwa katika rasimu ya sheria inayosimamia watu na familia.
Katika maelezo ya muswada huo, serikali imeonyesha kuwa wakati wa mashauriano, ilipendekezwa kwamba umri wa kuolewa urekebishwe hadi miaka 18 kwani, katika umri huo, mtu ana haki ya kufanya mapenzi lakini hawezi kuolewa kisheria.
"Rasimu hii ya sheria inapendekeza kwamba mtu aliye na umri wa kuoa lakini bado hajatimiza umri wa kuolewa, anaweza kuomba idhini ya kuoa, kwa sababu zinazoeleweka, kwa msajili wa serikali katika ngazi ya wilaya," maelezo ya muswada huo yanasema.
Kulingana na sheria ya Rwanda utu uzima unaanzia miaka 18. Hii ina maana kwamba mtu yeyote ambaye amefikia umri huo anaweza kuingia mkataba, ana haki ya kushtaki au kushtakiwa, pamoja na kuwajibika kisheria endapo atafanya uhalifu, kwani yeye si mtoto tena.