Serikali ya Rwanda inasema kuwa imewakamata wanajeshi kutoka jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, linalojulikana kama FARDC.
"Leo asubuhi saa 0110, askari watatu wenye silaha kutoka DRC na kuingia Rwanda katika Wilaya ya Rubavu (katika eneo ya Rubavu/Kiini cha Rukoko/Kijiji cha Isangano)," imesema taarifa kutoka Jeshi la Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi hao walikamatwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Rwanda.
"Wawili kati ya askari hao, Sajenti Asman Mupenda Termite (miaka 30) na Koplo Anyasaka Nkoi Lucien (miaka 28), walikamatwa na askari wa doria wa RDF wakisaidiwa na walinzi wa kitongoji cha eneo hilo (Irondo)," taarifa ya jeshi imeongeza.
Taarifa hiyo ilidai kuwa wanajeshi hao walikutwa na silaha tofauti, ikiwemo AK-47 iliyokuwa na risasi, fulana maalumu ya kuzuia risasi na mifuko iliyojaa bangi.
"Askari wa tatu alipoteza maisha baada ya kushambuliwa na wanajeshi hao waliokuwa lindoni. Hakuna askari wa Rwanda aliyejeruhiwa kwenye shambulizi hilo," taarifa hiyo ilisema,
Wakati serikali ya Rwanda ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo, hakuna kauli yoyote kutoka kwa DRC.