Zoezi hilo ambalo lilikuwa lifanyike Oktoba 8, limeahirishwa kwa mujibu wa Bodi ya Maendeleo ya nchi hiyo.
Kulingana na taarifa kwa umma iliyotolewa na bodi hiyo, mchakato huo umeahirishwa hadi hapo utakapotangazwa tena.
Takribani sokwe 22 wangepewa majina kwenye makala ya 20 ya zoezi maarufu lijulikanalo kama Kwita Izina, ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika Oktoba 18 mwaka huu.
Kama kawaida, shughuli hiyo ilikuwa ifanyike kwenye Hifadhi ya Taifa ya milima ya volcano iliyoko kwenye wilaya ya Musanze nchini Rwanda.
Zoezi la kuwapa majina wanyama hao, lilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2005, ambapo hadi kufikia sasa, sokwe wadogo wapatao 395 wamepewa majina, mchakato ambao unatazamiwa kukuza sekta ya utalii nchini humo, kulingana na Afisa Utalii wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Michaella Rugwizangoga.
Watu maarufu wakiwemo wachezaji nyota wa soka, wanamuziki na wadau wengine muhimu kwenye sekta utalii walitarajiwa kushuhudia tukio hilo.
Utalii wa sokwe nchini Rwanda huchangia asilimia moja ya pato la taifa la Rwanda, ikiwa ni sekta muhimu kwa maendeleo ya jamii.