Kulingana na serikali ni asilimia tisa tu ya wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi nchini Rwanda wanaoshughulikiwa na mpango wa malipo ya uzeeni.

Vyama vya wafanyakazi nchini Rwanda vimeitaka serikali kuweka kipaumbele katika nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi ili waweze kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.

Wawakilishi hao wa wafanyakazi wanasema mishahara iongezwe kabla ya serikali kuzingatia mapendekezo ya nyongeza ya michango ya mafao ya uzeeni.

Maoni yao yanakuja wakati kuna pendekezo la serikali la kufanya mageuzi ya mafao ya uzeeni ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza Januari 2025.

Mapendekezo hayo, yanajumuisha kuongeza michango ya kila mwezi ya mafao ya uzeeni kutoka asilimia 6 ya sasa ya mshahara wa msingi wa kila mwezi wa mfanyakazi hadi asilimia 12 ya jumla ya mshahara wake wa kila mwezi.

Novemba 2024 Serikali ilitangaza kuwa raia wa Rwanda walioajiriwa katika sekta rasmi wataanza kulipwa asilimia 12 ya mishahara yao ya kila mwezi, kutoka asilimia sita ya sasa, kama sehemu ya mageuzi ya pensheni yanayotarajiwa kuanza Januari 2025. Bodi ya Hifadhi ya Jamii ya Rwanda (RSSB) ilisema michango ya mafao ya uzeeni itagawanywa kwa usawa kati ya mwajiri na mwajiriwa kama ilivyo sasa. Marekebisho hayo yanahusu wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi.

Kwa sasa, kiwango cha jumla cha michango kimewekwa katika asilimia sita ya mshahara wa msingi wa mfanyakazi, huku mwajiri na mwajiriwa wakichangia asilimia 3 kila mmoja.

“Hata hivyo, inafika wakati tumekuwa tukionyesha kwamba kuna haja ya marekebisho ya mishahara ili kuendana na bei sokoni," alisema Africain Biraboneye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Rwanda (CESTRAR)

"Kuongezeka kwa kiwango cha mchango [wa pensheni] kutasababisha kupunguzwa kwa malipo madogo ambayo mfanyakazi amekuwa akipokea, ambayo itaathiri hali ya maisha," aliongezea Biraboneye.

Vyama vya wafanyikazi vilielezea wasiwasi wao juu ya ukosefu wa mashauriano kati ya serikali na wawakilishi wa wafanyakazi ili watoe maoni kwa mabadiliko yaliyopendekezwa.

"Wakati mshahara wa mfanyakazi ni mdogo, hawatapata mafao makubwa ya kustaafu," alisema Eric Nzabandora, rais wa Chama cha Labour Congress na Udugu wa Wafanyakazi nchini Rwanda (COTRAF Rwanda).

Ameongezea kuwa wamekuwa wakitetea kuweka kiwango cha chini cha mshahara ambacho kinakidhi hali halisi ya maisha lakini hii bado halijafanyika.

Kulingana na Serikali ni asilimia tisa tu ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi nchini Rwanda wanaofaidika na mpango wa malipo ya uzeeni. Hii ina maana kwamba takriban asilimia 90 ya watu wanaofanya kazi nchini Rwanda wameajiriwa katika sekta isiyo rasmi na kwa hiyo wako nje ya mpango huo.

TRT Afrika