Rais Kagame wa Rwanda asema atawania muhula wake wa nne / Picha: AFP

Ni mara ya kwanza Kagame kuweka wazi nia yake tangu Rwanda iliposhuhudia marekebisho ya kikatiba mnamo 2015 huku yakimruhusu kuwania mihula zaidi na kusalia madarakani hadi 2034.

"Ndiyo, nitagombea," Kagame, aliiambia gazeti la habari la lugha ya kifaransa, Jeune Afrique, katika mahojiano yaliyochapishwa mtandaoni siku ya Jumanne.

Mapema mwezi Machi, Serikali ya Rwanda iliziunganisha tarehe za uchaguzi wake wa bunge na urais, unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka ujao, 2024.

"Nimefurahishwa na imani Wanyarwanda walioweka ndani yangu. Nitawahudumia kila wakati na ninaweza, " kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 alinukuliwa akisema.

Kagame, ambaye ni kiongozi wa zamani wa waasi, alipata urais Aprili 2000 lakini amekuwa akionekana kama kiongozi wa nchi hiyo tangu mwisho wa mauaji ya kimbari ya 1994.

Mnamo 2022 alipoulizwa kama angejaribu kusaka kuchaguliwa tena, Kagame alisema "atafikiria kuwania kwa miaka mingine 20".

Kagame alirudishwa madarakani ofisini kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura katika uchaguzi wa 2003, 2010 na 2017.

AFP