Philippe Mpayimana anawania Urais wa nchi kama mgombea binafsi./Picha: TRT Afrika

Wakati kampeni za uchaguzi wa zikiendelea kushika kasi nchini Rwanda, mgombea binafsi anayewania nafasi ya uongozi wa juu wa nchi hiyo, Phillippe Mpayimana ameazimia kupunguza idadi ya wabunge na mawaziri, iwapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi hiyo.

Mpayimana, ambaye anawania kiti hicho dhidi ya Rais Paul Kagame kutoka Rwanda Patriotic Front (RPF Inkotanyi) na Frank Habineza anayewakilisha DGPR, amesema kuwa analenga kupunguza idadi ya wabunge na mawaziri kutoka 80 hadi 65.

Kulingana na mwanasiasa huyo, ni lazima kwa wagombea wa nafasi za ubunge kufanya kampeni zao kuanzia ngazi ya wilaya.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Kigali Juni 25, Mpayimana alisema kuwa utaratibu uliopo hivi sasa ambapo vyama huwapigia debe wagombea wao kupitia asasi hizo za kisiasa si njia bora ya kuwachagua wawakilishi wa wananchi bungeni.

Hii ni mara ya pili kwake kugombea nafasi hiyo ya juu nchini Rwanda baada ya kujaribu hivyo mwaka 2017 na kuambulia asilimia 0.72 ya kura zote kwenye uchaguzi ambao Rais Paul Kagame alishinda kwa kishindo.

Nchi ya Rwanda inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Julai 15, 2024, uchaguzi wake wa nne toka machafuko ya mwaka 1994, yalioua Watutsi na Wahutu 800,000 mwaka 1994.

TRT Afrika